Umoja wa Afrika waifungia milango Sudan
27 Oktoba 2021Umoja huo umesema unaipinga hatua ya jeshi ya kutwaa madaraka kwa nguvu ambayo umeitaja kuwa ni kinyume cha katiba.
Umoja huo umesema kupitia taarifa yake kwamba kwa pamoja wanalaani vikali hatua ya jeshi ya kutwaa madaraka kwa nguvu na kutamka rasmi kusitisha uanachama wake kwenye umoja huo.
Hii ni mara ya pili baada ya mwezi Juni, Sudan kusimamishwa uanachama na Umoja wa Afrika baada ya kuwauwa waandamanaji waliokuwa wakishinikiza utawala wa kiraia, nje ya makao makuu ya jeshi nchini humo, na kurejeshewa miezi mitatu baada ya kutangazwa kwa baraza la kwanza la mawaziri tangu kuondolewa kwa aliyekuwa kiongozi wa taifa hilo, Omar al-Bashir.
Soma Zaidi: Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuijadili Sudan
Wakati Umoja huo ukitangaza hatua hiyo, Benki ya Dunia nayo imesema leo kwamba inasitisha misaada kwa Sudan kufuatia mzozo huo wa kisiasa.
Rais wa Benki ya Dunia, David Malpass, amesema kwenye taarifa yake kwamba ana wasiwasi mkubwa kutokana na matukio hayo ya karibuni nchini Sudan na kuelezea hofu yake kuhusiana namna mzozo huo utakavyoathiri pakubwa mchakato wa kufufua upya uchumi wake ulioathiriwa vibaya na vikwazo vya kimataifa na matumizi mabaya, wasiwasi unaoungwa mkono na wachambuzi.
Mataifa mengi ya magharibi yaitishia Sudan.
Pamoja na Benki ya Dunia, Marekani imekwishazuia kwa muda msaada wake wa dola milioni 700 kwa Sudan, huku Ujerumani ikitishia kukata misaada iwapo serikali ya kiraia haitarudishwa mara moja.
Tayari mataifa kadhaa ya magharibi yametoa mwito wa kufanyika kwa mkutano wa dharura na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Sudan, Abdallah Hamdok yakisema bado yanamtambua kikatiba kiongozi huyo pamoja na baraza lake. Kwenye taarifa mapema leo balozi za Umoja wa Ulaya, Marekani, Uingereza, Ufaransa na mataifa mengine ya Ulaya wametoa mwito wa kuachiwa kwa maafisa wanaoshikiliwa na kufanyika kwa mazungumzo kati ya jeshi na vuguvugu linalounga mkono demokrasia.
Jeshi laingia mtaani kuwadhibiti waunga mkono demokrasia.
Lakini pamoja na vitisho hivyo vya mataifa na taasisi zenye nguvu ulimwenguni vikiendelea kutolewa dhidi ya Sudan, mchana huu kuliripotiwa kwamba jeshi limeanzisha operesheni pana kabisa ya kuwakamata waandamanaji wanaopinga mapinduzi hayo ya kijeshi.
Soma Zaidi: Mamia wapinga kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Sudan
Jeshi hilo limetawanya idadi kubwa ya askari baada ya maandamano yaliyoshuhudiwa usiku kucha na kugubikwa na makabiliano kati ya waandamanaji na wanajeshi katika mji mkuu, Khartoum. Mmoja ya waandamanaji ameliambia shirika la habari la AFP kwamba polisi waliondoa vizuizi vyote vilivyowekwa barabarani kuanzia mapema leo na kumkamata kila aliyekuwa karibu na vizuizi hivyo.
Tangu Jenerali Abdel Fattah al-Burhan alipotangaza kuivunja serikali na hali ya dharura, maelfu ya raia wameendelea kuandamana, wakiupinga utawala wa kijeshi.
Waziri mkuu aliyepinduliwa Sudan, Abdullah Hamdok, amerudishwa nyumbani kwake na ulinzi mkali umewekwa. Kwa mujibu wa wasaidizi wake yuko nyumbani kwake pamoja na mkewe.Waziri Mkuu wa Sudan arejeshwa nyumbani
Mashirika: APE/AFPE