Umoja wa Afrika waisimamisha uanachama Cote d'Ivoire.
10 Desemba 2010Uamuzi huo wa Umoja wa Afrika umekuja baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na viongozi wa Kiafrika kusema kwamba bwana Gbagbo anapaswa kuachana na juhudi zake za kung'ang'ania madaraka, baada ya duru ya pili ya uchaguzi nchini humo iliyompa ushindi mpinzani wake Allasane Ouattara.
Mkuu wa Tume ya Afrika inayoshughulika na masuala ya ulinzi na Usalama katika Umoja wa Afrika Ramtane Lamamra amewaambia waandishi wa habari katika makao makuu ya umoja huio, mjini Addis Ababa Ethiopia, kwamba uamuzi huo uliochukuliwa wa kuisimamisha Cote d'Ivoire kushiriki katika shughuli za umoja huo mpaka pale rais aliyechaguliwa kidemokrasia Alassane Ouattara atakaposhika madaraka.
Uamuzi huo wa jumuia hiyo yenye wanachama 53, unaongeza kutengwa kwa bwana Gbagbo, huku Marekani nayo ikionya kuweka vikwazo.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani Philip Crowley, amesema barua ya Rais wa nchi hiyo Barack Obama aliyomwandikia bwana Gbagbo imeweka wazi kwamba iwapo anafanya uamuzi usio sawa, wataweza kumuwekea vikwazo na watu wake wengine ikiwa ni lazima kufanya hivyo.
Na katika hatua nyingine, serikali iliyoanzishwa na kiongozi wa upinzani Alassane Ouattara imelitolea wito jeshi la nchi hiyo kumtambua kiongozi huyo kama mkuu wa nchi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na serikali ya Bwana Ouattara, serikali inahitaji kwamba majeshi ya ulinzi na usalama kuweka utii wake kwa Rais Alassane Ouattara, ambaye ndiye mkuu wa majeshi.
Aidha taarifa hiyo pia imetaka kuongeza juhudi za kumbana bwana Gbagbo ambaye anakabiliwa ongezeko la kutengwa na jumuia ya kimataifa ikiwemo baraza la usalama la umoja wa mataiafa, Umoja wa Afrika na jumuia nyingine za kikanda, kwa lengo la kumshinikiza aachie madaraka.
Awali upande unaoongozwa na Bwana Ouattara wiki hii ulipanga kuanza kufanya kazi zake ilizokusudia, lakini umekwama kutokana na hatua hiyo ya Bwana Gbagbo.
Aidha upande huo pia maafisa na mashirika yote ya serikali kuacha mara moja kufanya kazi na serikali isiyo halali ya Bwana Gbagbo na kusubiri kupata maelekezo kutoka kwa Waziri mkuu mpya aliyechaguliwa katika baraza jipya la upinzani Guillaume Soro.
Wakati huohuo, Waziri wa ulinzi wa Ufaransa Alain Juppe amesema nchi yake iko katika tahadhari ya kuwahamisha maelfu ya raia wake, katika nchi hiyo ambayo zamani ilikuwa koloni lake, iwapo hali itazidi kuwa mbaya.
Mwandishi: Halima Nyanza(afp, Reuters)
Mhariri:Mwadzaya,Thelma