1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Umoja wa Afrika wakutana kuijadili Sudan

16 Aprili 2023

Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika limeitisha kikao cha dharura hii leo kujadiliana hali ya kisiasa na usalama nchini Sudan.

https://p.dw.com/p/4Q9vj
Sudan | Sudanesische Soldaten der Rapid Support Forces-Einheit
Picha: Hussein Malla/AP/picture alliance

Jeshi la Sudanna kikosi maalumu cha wanamgambo cha Rapid Support Forces, RSF wameendelea kwa siku ya pili kupambania  udhibiti wa taifa hilo, hali inayoashiria kutokuwa tayari kumaliza uhasama licha ya kuongezeka kwa shinikizo la kidiplomasia la kusitisha mapigano.

Mapigano makali ya ardhini na angani yameshuhudiwa hii leo katika mji mkuu, Khartoum na mji unaopakana nao wa Omdurman pamoja na maeneo mengine yanayozozaniwa nchini humo.

Kulingana na Kamati Kuu ya madaktari nchini Sudan, watu 56 wameuawa ikiwa ni pamoja na watumishi watatu wa shirika la Mpango wa chakula ulimwenguni, WFP. Shirika hilo limetangaza kusitisha kwa muda shughuli zake nchini humo. Umoja wa Mataifa umelaani mauaji ya watumishi hao waliokuwa wakitekeleza majukumu yao.

Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika limeitisha kikao cha dharura hii leo kujadiliana hali ya kisiasa na usalama nchini Sudan, hii ikiwa ni kulingana na taarifa kupitia ukurasa wa Twitter.

Katika hatua nyingine, Misri kupitia mwakilishi wake kwenye Muungano wa mataifa ya Kiarabu, imezitaka pande zinazohasimiana kuhakikisha usalama wa maslahi yake.