1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Afrika 'wasikitishwa' na Marekani kujiondoa WHO

22 Januari 2025

Umoja wa Afrika umeonyesha kusikitishwa Jumatano kutokana na uamuzi wa Rais Donald Trump wa kuiondoa Marekani kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), ukihimiza utawala wake kufikiria upya uamuzi huo.

https://p.dw.com/p/4pTsP
John Nkengasong | Mkurugenzi wa Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika (Africa CDC)
Mkurugenzi wa Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika (Africa CDC)Picha: Mulugeta Ayene/AP/picture alliance

Saa chache tu baada ya kuingia madarakani Jumatatu, Trump alisaini amri ya kiutendaji ya kuelekeza Marekani kujiondoa kutoka shirika hilo la Umoja wa Mataifa, hatua inayotishia kuacha miradi ya afya ya kimataifa bila ufadhili wa kutosha.

Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, alisema katika taarifa kwamba alisikitishwa "kusikia tangazo la serikali ya Marekani la kujiondoa" kutoka WHO yenye makao yake mjini Geneva.

Washington ni mchangiaji mkuu wa kifedha kwa shirika hilo, na kujiondoa huko kunakuja wakati Afrika inakabiliwa na changamoto mbalimbali za kiafya, ikiwemo milipuko ya hivi karibuni ya virusi vya mpox na Marburg.

Virusi vya Marburg ni hatari kiasi gani?

"Sasa zaidi ya wakati wowote, dunia inategemea WHO kutekeleza jukumu lake la kuhakikisha usalama wa afya ya umma kimataifa kama faida ya pamoja," alisema Moussa Faki, akiongeza kuwa ana matumaini "serikali ya Marekani itafikiria upya uamuzi wake."

Alisema Washington ilikuwa miongoni mwa waungaji mkono wa mwanzo wa CDC ya Afrika, kitengo cha afya cha Umoja wa Afrika ambacho kinashirikiana na WHO kukabiliana na milipuko ya sasa na inayojitokeza.

Soma pia: WHO yaendelea na uchunguzi wa ugonjwa usiojulikana Kongo

Trump ameikosoa WHO mara kwa mara kutokana na jinsi ilivyoshughulikia janga la Covid-19 na alisema kabla ya kuapishwa kuwa "WHO ilitutapeli."

Marekani ilikuwa katika mchakato wa kujiondoa kutoka WHO wakati wa muhula wa kwanza wa Trump, lakini hatua hiyo ilifutwa chini ya utawala wa Joe Biden.

Tom Frieden, afisa wa zamani wa ngazi ya juu wa afya wa Marekani, aliandika kwenye X kwamba kujiondoa huko "kunadhoofisha ushawishi wa Marekani, kunaongeza hatari ya janga hatari, na kupunguza usalama wa wote."

Fahamu zaidi kuhusu ugonjwa wa Parkinson

Hii inajiri wakati hofu inazidi kuhusu uwezekano wa mlipuko wa homa ya mafua ya ndege, ambayo imeathiri watu kadhaa na kusababisha kifo cha kwanza cha binadamu nchini Marekani mapema mwezi huu.

Nchi wanachama wa WHO zimekuwa zikijadiliana mkataba wa kwanza wa dunia wa kushughulikia milipuko ya baadaye tangu mwishoni mwa 2021 — majadiliano ambayo sasa yataendelea bila Marekani.