1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Afrika yataka madaraka yagawanywe nusu kwa nusu Zimbabwe

Mohamed Dahman2 Septemba 2008

Tanzania ambayo inashikilia uwenyekiti wa Umoja wa Afrika inataka kuona kufikiwa haraka kwa makubaliano ya kushirikiana madaraka nchini Zimbabwe ambapo madaraka hayo yatakuwa yamegawanywa nusu kwa nusu.

https://p.dw.com/p/FADu
Kusambaratika kwa uchumi kumepelekea maduka mengi kuwa matupu bila ya bidhaa nchini Zimbabwe.Picha: AP

Chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe cha MDC kimesema mazungumzo na chama cha ZANU-PF cha Rais Robert Mugabe ambayo yalianza tena hapo Ijumaa nchini Afrika Kusini yameshindwa kufikia makubaliano.

Waziri wa mambo ya nje wa Tanzania Bernard Membe amesema mjini Dar-es-Salaam leo hii kwamba kuna tatizo na watataraji upatanishi utaendelea na kwamba busara itatumika.

Membe amewaambia waandishi wa habari katika mji huo mkuu wa kibiashara kwamba wangelipendelea uvumbuzi upatikane mara moja kutokana na kupamba moto kwa mzozo wa kiuchumi na kwamba bado wataendelea kuomba kwamba suluhisho lipatikane chini ya msingi wa kugawana madaraka nusu kwa nusu.

Hapo Ijumaa wapatanishi kutoka chama cha ZANU-PF chama kikuu cha upinzani cha MDC na kundi dogo lililojitenga na chama hicho walikutana kwa nyakati tafauti na Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini ambaye ni msuluhishi wa mazungumzo hayo.

Mazumngumzo hayo ya kushirikana madaraka yamekwama juu ya namna ya kugawana madaraka makuu ya utendaji kati ya Mugabe na kiongozi wa chama cha MDC Morgan Tsvangirai ambaye aligoma kusaini makubaliano hayo wiki mbili zilizopita ambayo yangelimfanya kuwa waziri mkuu.

Tsvangirai alipinga makubaliano hayo yaliopendekezwa kwa kusema kwamba hayakumpa madaraka ya kutosha ya utendaji.

Kiongozi huyo wa upinzani hapo mwezi wa Julai alimshinda Mugabe katika uchaguzi wa tarehe 29 mwezi wa Machi lakini alishindwa kupata kura za kutosha kuepuka marudio ya uchaguzi huo wa rais ambao Mugabe alishindwa bila ya mpizani baada ya Tsvangirai kujitowa kwa kile alichokisema kwamba vitendo vya umwagaji damu na vitisho dhidi ya wafuasi wake.

Kugharamika kwa uchumi wa nchi hiyo kunaongezeka kila siku kutokana na kukwama kwa mazungumzo hayo.

Shida ikiwa ni pamoja na kupanda kwa gharama za maisha kwa zaidi ya asilimia milioni 11 ambacho ni kiwango cha juu kabisa duniani tayari kumesababisha mamilioni ya Wazimbabwe kukimbilia katika nchi jirani.

Wahakiki wanasema sera za Mugabe kama vile za kunyakuwa mashamba ya biashara yanayomilkiwa na wazungu na kuyakabidhi mashamba hayo kwa wazalendo kumeangamiza sekta ya kilimo ya nchi hiyo ambayo huko nyuma ilikuwa ikinawiri.

Mugabe ambaye amekuwa madarakani tokea Zimbabwe ijipatie uhuru wake kutoka Uingereza hapo mwaka 1980 analaumu vikwazo vya mataifa ya magharibi kwa kuusambaratisha uchumi wa nchi hiyo.

Wakati huo huo Zimbabwe imeweka masharti mapya makali kwa mashirika ya misaada ya kibinaadamu yanayoendesha shughuli zake nchini humo kufuatia kuondolewa kwa marufuku dhidi yao wiki iliopita.

Gazeti la serikali la The Herald limeripoti kwamba katika kipindi cha usoni mashirika yote ya misaada itabidi yawasilishe kwa ukamilifu mipango yao ya misaada ya kibinaadamu na michango ya fedha kadhalika maeneo na muundo wa shughuli zao kwa serikali.

Hapo Ijumaa Zimbabwe iliondowa marufuku kwa mashirika ya misaada yaliopigwa marufuku kabla ya marudio ya uchaguzi wa rais wa tarehe 27 mwezi wa Juni kwa tuhuma kwamba baadhi yao yalikuwa yakishirikiana na upinzani.