1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaNiger

Hali ya usalama Afrika Magharibi na Sahel inazidi kuzorota

26 Julai 2023

Ofisi ya Umoja wa Mataifa katika eneo la Afrika Magharibi na ukanda wa Sahel imesema hali ya usalama katika maeneo hayo inazidi kuzorota, huku kukiwa na mashambulizi mengi dhidi ya raia na vikosi vya ulinzi na usalama.

https://p.dw.com/p/4UOOe
Zentralgefängnis Guinea Conakry
Wanajeshi wa kikosi maalum cha GuineaPicha: CELLOU BINANI/AFP

Kauli hiyo imetolewa Jumanne na mkuu wa ofisi hiyo Leonardo Santos Simao, wakati akizungumza katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Simao amesema mazingira ya usalama kwenye maeneo hayo ni magumu, na ili amani ya kudumu iweze kupatikana, panahitajika msaada halisi na wa muda mrefukutoka katika ukanda huo na kimataifa. Simao amesema watu milioni 6.3 wameyakimbia makaazi yao katika ukanda wa Sahel na ametoa wito kwa wadau wote kusaidia katika kuzingatia utu wa wakimbizi na usalama wa nchi zinazowahifadhi.

Mwakilishi huyo wa Umoja wa Mataifa amesema idadi hiyo ya wakimbizi inakumbusha wajibu wao wa pamoja kuunga mkono juhudi na mpango kazi wa nchi za Afrika Magharibi katika kutatua migororo, kutokomeza ugaidi, na kukomesha ukosefu wa usalama katika eneo la Sahel.

Afrika Magharibi imerekodi mashambulizi 1,800 ya kigaidi 

Wakati huo huo, Rais wa Kamisheni ya Jumuiya ya Uchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, Omar Alieu Touray, amesema Afrika Magharibi imerekodi zaidi ya mashambulizi 1,800 ya kigaidi katika miezi sita ya kwanza ya mwaka 2023. Touray ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba mashambulizi hayo yamesababisha takribani vifo 4,600 na matokeo mabaya ya kiutu.

Amesema vifo 4,593 vimetokana na mashambulizi ya kigaidi kati ya Januari na Juni 30, ikijumuisha vifo 2,725 vilivyotokea Burkina Faso, 844 Mali, 77 Niger na 70 Nigeria.

Afrika ECOWAS Gipfel
Viongozi wa ECOWAS wakihudhuria moja ya mikutano ya jumuia hiyoPicha: FRANCIS KOKOROKO/REUTERS

Kwa mujibu wa Touray watu nusu milioni katika mataifa 15 ya ECOWAS ni wakimbizi na takribani milioni 6.2 ni wakimbizi wa ndani. Amesema hiyo ni sehemu ndogo tu ya madhara ya kutisha ya ukosefu wa usalama, na ameonya kuwa mamilioni ya watu wanahitaji msaada wa chakula, kwa sababu mapigano yamesababisha ukosefu wa chakula.

''Tathmini yetu inaonyesha kuwa takribani watu milioni 30 wanahitaji msaada wa chakula. Iwapo jumuia ya kimataifa haitolishughulikia hilo, idadi ya watu wanaohitaji msaada wa chakula itaongezeka kutoka milioni 30 hadi milioni 42 ifikapo mwishoni mwa mwezi ujao,'' alifafanua Touray.

Rais huyo wa Kamisheni ya ECOWAS amesema ukosefu wa usalama kwenye eneo la ECOWAS unasababishwa na ugaidi, uasi wa kutumia silaha, uhalifu uliopangwa, mabadiliko ya serikali kinyume na katiba, shughuli haramu za baharini, mizozo ya mazingira, pamoja na taarifa za uongo. Amesema ukanda huo una wasiwasi juu ya kuibuka tena kwa mapinduzi ya kijeshi, huku nchi tatu za Mali, Burkina Faso na Guinea zikiwa zinatawaliwa kijeshi.

Kauli za Marekani na Urusi

Naibu balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Robert Wood, ameliambia Baraza la Usalama la umoja huo kwamba nchi yake bado ina wasiwasi mkubwa kutokana na kuporomoka kwa demokrasia katika eneo lote la Afrika Magharibi na Sahel, na inasikitishwa sana na kukosekana kwa utulivu.

Naye naibu balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Anna Evstigneeva amesema hali ya usalama Afrika Magharibi na Sahel ni ngumu, akitolea mfano kuongezeka kwa shughuli za wapiganaji wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS na harakati za uasi za Boko Haram.

(AP)