1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa hatiani kuhusu unyanyasaji wa kingono DRC

Saleh Mwanamilongo
29 Septemba 2021

Shirika la Afya Duniani,WHO limesema wafanyakazi wa mashirika ya misaada waliwanyanyasa kingono wanawake wakati wa mripuko wa ugonjwa wa Ebola nchini Congo.

https://p.dw.com/p/411yT
WHO-Chef | Tedros Adhanom Ghebreyesus
WHO | Tedros Adhanom GhebreyesusPicha: Fabrice Coffrini/REUTERS

Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema amesikitishwa na madai hayo yaliyofanywa kati ya mwaka 2018 na 2020 na ameomba radhi.

"Lazima tuchukue hatua mara moja, na tutawajibika, katika nafasi tatu. Kwanza, ni msaada, ulinzi na haki kwa waathirika na wanusura; Pili ni hatua za kushughulikia usimamizi na kushindwa kwa wafanyikazi na Tatu ni mageuzi ya jumla ya miundo na utamaduni wetu",alisema Gebreyesus.

Tume hiyo ilizungumza na wanawake 63 na wanaume 12 walioathiriwa. Madai hayo yalijulikana mwaka mmoja baada ya uchunguzi wa shirika la habari za masuala ya kibinaadamu na taasisi ya Thomson Reuters. Unyanyasaji huo haukufanywa tu na mashirika ya Umoja wa Mataifa kama vile WHO, la kuwahudumia Watoto, UNICEF na la Wahamiaji, IOM, lakini pia mashirika ya misaada kama vile Oxfam, madaktari wasio na mipaka, World Vision na ALIMA.

Soma pia:Mfumo wa afya DRC dhidi ya Ebola haukuwasaidia raia 

''Niliona yote kwa mecho yangu mwenyewe''

Uchunguzi ulibaini jumla ya madai tisa ya ubakaji
Uchunguzi ulibaini jumla ya madai tisa ya ubakajiPicha: Carol Valade/AFP/Getty Images

Mmoja ya waathiriwa, mwanamke ambaye alikuwa mfagiaji katika kituo cha huduma ya wagonjwa wa Ebola,mjini Butembo amesema alilazimishwa kufanya mapenzi na mfanyakazi wa shirika la WHO kabla ya kupewa ajira hiyo.

''Sio mimi tu ambaye nimefanyiwa hivyo! Nina wanawake wenzangu kadhaa ambao walikwenda kulala na watu, walifanya mapenzi, na kisha kupewa ajira baada ya kitendo hicho. Niliona yote kwa macho yangu mwenyewe, nika yahisi kwenye mwili wangu mwenyewe.''

Malick Coulibaly, mwanachama wa jopo huru la uchunguzi amesema uchunguzi ulibaini jumla ya madai tisa ya ubakaji. Wanawake waliohojiwa walisema washambuliaji wao hawakutumia udhibiti wa uzazi, na kusababisha mimba zingine.Coulibaly amesema wanawake wengine walisema wabakaji wao waliwalazimisha kutoa mimba.

Soma pia:Tedros mgombea pekee WHO licha ya kupingwa na Ethiopia

Umoja wa Mataifa kuwajibika

Msichana aliyejitambulisha kwa jina la Joliana, ambaye ni moja ya wathirika alikuwa na umri wa miaka 13 tu wakati alipobakwa na wafanyakazi hao wa Umoja wa Mataifa.

Mkuu wa shirika la WHO amesema watu wanne wamefukuzwa kazi na wawili kuachishwa kazi kwa muda kama matokeo mwanzo ya kashfa hiyo, lakini hakuwataja majina. Tedros Gebreyesus  pia alikataa kusema ikiwa atafikiria kujiuzulu.

Wiki iliopita Ujerumani, Ufaransa na nchi nyingine kadhaa za Ulaya zilimteua Tedros kwa muhula wa pili kama kiongozi wa shirika la WHO.