1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa kuijadili Myanmar Jumatano

29 Machi 2021

Uingereza imetoa mwito wa kuitishwa kwa kikao cha dharura cha baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuzungumzia hali ilivyo nchini Myanmar ambako mamia ya waandamanaji wanaoyapinga mapinduzi.

https://p.dw.com/p/3rLWJ
USA Sicherheitsrat der Vereinten Nationen Friedensverhandlungen in Kolumbien
Picha: picture-alliance/dpa/M. Rajmil

Uingereza imetoa mwito wa kuitishwa kwa kikao cha dharura cha baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuzungumzia hali ilivyo nchini Myanmar ambako mamia ya waandamanaji wanaoyapinga mapinduzi kuuawa mwishoni mwa wiki iliyopita. Haya yanajiri wakati mashambulizi ya anga nchini humo yakizidi kutishia hali ya usalama. 

Kulingana na duru za kidiplomasia, baraza hilo la usalama lenye wajumbe 15 litaanza kwa vikao vya ndani siku ya Jumatano na mjumbe maalumu wa Myanmar katika Umoja huo Christine Schraner Burgener ataliarifu kuhusu hali ilivyo nchini humo.  

Msururu wa mashambulizi ya anga kwenye eneo lote la mpaka nchini Myanmar umeibua wasiwasi mkubwa na huenda wakaazi wengi eneo hilo wakakimbilia nchini jirani Thailand.

Myanmar | Protest in Yangon
zaidi ya waandamanaji 100 wameuawa nchini Myanmar kufuatia hatua kali za jeshiPicha: AP Photo/picture alliance

Siku ya Jumamosi, zaidi ya waandamanaji 100 waliuawa kote nchini Myanmar, idadi ambayo ni kubwa zaidi kuwahi kutokea kwa siku moja tangu kulipoanza maandamano hayo.

Mjumbe wa shirika la huduma za kibinaadamu la Free Burma Rangers Dave Eubank amesema ndege za kijeshi la Myanmar zimefanya mashambulizi matatu ya angani usiku wa Jumapili na kumjeruhi vibaya mtoto mmoja na kusababisha wengine kukimbilia kaskazini mwa Thailand.

Waziri mkuu wa Thailand Prayut Chan-ocha amekiri kuhusiana na matatizo katika mpaka wa kaskazini mwa nchi hiyo na kusema serikali yake inajiandaa kupokea wakimbizi wengi kutokea Myanmar.

Ujerumani imelaani vikali matumizi ya nguvu yanayofanywa na jeshi na kutaka yaanchwe mara moja. Msemaji wa serikali Steffen Seibert akiwa mjini Berlin amesema ni bahati mbaya kwamba matumizi hayo ya nguvu yamefikia kiwango cha kusikitisha mno. 

"Serikali ya Shirikisho inalaani vikali matumizi ya nguvu yanayofanywa na usalama vya Myanmar na matumizi mabaya ya silaha. Matukio haya ya kikatili kwa bahati mbaya yalifikia kiwango cha kusikitisha mwishoni mwa wiki. Hakuna sababu ya kutumia nguvu ya kuwaua watu wanaoandamana kwa amani, kama ilivyotokea tena mwishoni mwa wiki hii."

USA Joe Biden | Erste PK im Weißen Haus
Rais Joe Biden wa Marekani amekuwa miongoni mwa wakuu waliolaani mashambulizi hayo ya MyanmarPicha: Chip Somodevilla/Getty Images/AFP

Rais wa Marekani Joe Biden amelaani vikali matukio hayo ya mwishoni mwa wiki akiyataja kuwa ni ya kutisha, wakati wawakilishi wa Umoja wa Mataifa wakilaani hatua hizo walizoziita mbaya na za kijinga zinazochukuliwa na jeshi la Myanmar. Biden amesema inaudhi sana hasa kutokana na ripoti anazozipata za watu kuuawa bila ya sababu za msingi.

Soma Zaidi:Vikosi vya usalama Myanmar vyaendeleza matumizi ya nguvu 

China kwa mara nyingine imeungana na miito ya kimataifa kuhusiana na wasiwasi unaoendelea, wakizitaka pande zote kujizuia. Japan na Indonesia pia wamelaani vikali hatua hizo.

Msemaji wa ikulu ya Urusi, Kremlin Dmitry Peskov amesema pamoja na kwamba wanaimarisha mahusiano na Myanmar, lakini wana wasiwasi mkubwa na hali ilivyo nchini humo.

Licha ya vifo hivyo, waandamanaji hii leo walifurika tena mitaani kote nchini humo na wengine wakitoa heshima zao mwisho kwa watu waliouawa.

Soma Zaidi: Wanaharakati watoa wito wa maandamano zaidi Myanmar

Mashirika: AFPE/APE