Umoja wa Mataifa kutuma kikosi Sudan Kusini
13 Agosti 2016Baraza lo usalama liliridhia azimio lililoandaliwa na Marekani na ambalo pia linatishia kuiwekea vikwazo vya silaha serikali ya Sudan Kusini iwapo itakizuia kikosi hicho. Nchi 11 kati ya 15 wanachama wa baraza hilo zilipiga kura kuliunga mkono azimio hilo. China, Urusi, Misri na Venezuela hazikupiga kura, zikisema zilishindwa kupata ridhaa ya Sudan Kusini kuhusiana na tume hiyo mpya.
Viongozi wa Umoja wa Afrika walitaka kikosi cha kikanda kuulinda mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba na kusaidia kuzilinda kambi za Umoja wa Mataifa mjini humo baada ya kuzuka machafuko yaliyosababisha vifo vya mamia ya watu mapema mwezi uliopita.
Ethiopia, Kenya na Rwanda zinatarajiwa kuchangia idadi kubwa ya wanajeshi katika kikosi hicho watakaokuwa na mamlaka kamili ya kutumia mbinu zote zitakazohitajika kutekeleza jukumu lao, ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua kali itakapohitajika.
Kikosi hicho kitahakikisha usalama mjini Juba na uwanja wa ndege na kwa haraka na kikamilifu kumkabili mtu yeyote atakayeonekana kujiandaa kufanya mashambulizi au kushiriki katika mashambulizi.
Kwa mujibu wa azimio hilo, baraza la usalama la Umoja wa Mataifa litatafakari kuiwekea vikwazo Sudan Kusini ikiwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ataripoti kwamba kuna vikwazo katika mchakato wa kukipeleka kikosi hicho. Ban atawasilisha ripoti kwa baraza la usalama katika siku 30 na kura kuhusu vikwazo huendea ikapigwa katika siku tano zitakazofuata iwapo atagundua kwamba serikali ya mjini Juba haitoi ushirikiano.
Vita vya Sudan Kusini vimeendelea kwa miaka miwili na nusu vikichochewa na mirundo ya silaha zinazoongezeka. Uingereza ilielezea kuvunjwa moyo kwamba vikwazo vya silaha havikuwekwa mara moja huku naibu balozi wa nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa, Peter Wilson, akiliambia baraza la usalama: "Lazima tulizingatie na tutaliangalia tena suala hili."
Sudan Kusini yapinga azimio
Kura hiyo ilifuatia wiki moja ya mashauriano magumu huku China, Urusi na Misri zikielezea wasiwasi wao kuhusiana na kuwatuma wanajeshi wa kuloinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini bila ridhaa kamili ya serikali.
Balozi wa Sudan Kusini katika Umoja wa Mataifa alisema serikali yake imelipinga azimio hilo, akiliambia baraza hilo kwamba taarifa za kina kuhusu kupelekwa kikosi hicho, ikiwa ni pamoja na muda na silaha watakazoruhusiwa wanajeshi kuzibeba ni masuala ambayo sharti yajadiliwe kwanza na serikali ya mjini Juba.
Uganda ambayo ni mshirika muhimu na wa karibu wa Sudan Kusini ilisema siku ya Ijumaa haitatuma wanajeshi katika kikosi hicho, huku shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumi wakimbizi, UNHCR, likiripoti kwamba raia 82,000 wa Sudan Kusini walikuwa wamevuka mpaka na kuingia Uganda katika wiki tano zilizopita.
"Hakuna mtu anayefikiri kwamba kikosi hiki cha kikanda kitakuwa suluhisho kwa hali ya kuyumba na machafuko yanayoendelea," alisema naibu balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, David Pressman. Lakini Pressman alisisitiza kwamba viongozi wa mataifa ya Afrika walikuwa wameomba ridhaa ya Umoja wa Mataifa kuwa na kikosi thabiti kuimarisha ulinzi na kuzifungulia mlango juhudi za kidiplomasia.
Mkataba wa amani uliodumu mwaka mmoja ulipata pigo wakati kiongozi wa zamani wa waasi Riek Machar alipokimbia kutoka mji mkuu Juba wakati wa mapigano. Miezi kadhaa ya juhudi za kidiplomasia zilisaidia Machar kurejea Juba mwezi Aprili 2016 kujiunga na serikali ya umoja wa kitaifa kama makamu wa kwanza wa rais.
Tume ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS, imekosolewa kwa kushindwa kuwalinda raia huku ikiwa na idadi ya wanajeshi 13,500 kwa sasa. Takriban raia 200,000 wa Sudan Kusini wamekuwa wakijihifadhi katika kambi za Umoja wa Mataifa kote nchini tangu vita vilipozuka Desemba 2013.
Shirika la kuwahudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR, lilisema kwa jumla zaidi ya watu milioni 2.5 wamelazimika kuyakimbia makazi yao wakati wa vita wakiwemo 93,000 waliokimbilia nchi jirani. Azimio la baraza la usalama lilirefusha mamlaka ya UNMISS hadi Desemba 15.
Mwandishi:Josephat Charo/afpe/ape
Mhariri:Sekione Kitojo