Umoja wa mataifa na Umoja wa Afrika wahimiza ufumbuzi wa Darfour upatikane haraka
6 Januari 2007New-York:
Umoja wa mataifa na Umoja wa Afrika wamepania kuzidisha juhudi za pamoja kuupatia ufumbuzi mzozo wa Darfour.”Utaratibu wa kisiasa katika eneo la mizozo kusini mwa Sudan unabidi ufufuliwe”-wamesema,mjumbe wa Umoja wa mataifa Jan Eliasson na muakilishi wa Umoja wa Afrika Salim Ahmed Salim,baada ya mazungumzo pamoja na katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki Moon.Mara baada ya kukabidhiwa wadhifa wake,katibu mkuu Ban alishadidia haja ya kushughulikiwa ipasavyo mzozo wa Darfour.Jimbo hilo la kusini magharibi ya Sudan limegubikwa na mapigano kati ya makundi tofauti ya wanamgambo wakiwemo Djanjawid wanaosaidiwa na serikali ya mjini Khartoum.Vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea tangu miaka mitatu iliyopita,vimeshagharimu maisha ya zaidi ya watu laki mbili na wengine zaidi ya milioni mbili na nusu wameyapa kisogo maskani yao.