Umoja wa Mataifa waanzisha medali ya Kapteni Mbaye Diagne
9 Mei 2014Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limeanzisha medali maalumu ya Kapteni Mbaye Diagne kuwaenzi wafanyakazi wa umoja huo watakaoonyesha ushujaa wa kiwango cha juu watakapokabiliwa na hatari kubwa katika kufanya kazi yao. Medali hiyo imepewa jina la kapteni wa Senegal ambaye bila kujihami na silaha na akikabiliwa na hatari kubwa dhidi ya maisha yake, aliwaokoa Wanyarwanda wapatao elfu moja wakati wa mauaji ya kimbari ya Rwanda dhidi ya Watutsi mnamo mwaka 1994.
Azimio hilo lililopendekezwa na Jordan na kuungwa mkono bila kupingwa, linatambua kwa masikitiko na majuto makubwa kabisa kwamba familia ya kapteni Diagne haikupokea ujumbe wowote wa shukurani kutoka makao makuu ya Umoja wa Mataifa baada ya kifo chake. Balozi wa Jordan katika Umoja wa Mataifa, Mwanamfalme Zeid Ra'ad Zeid al-Hussein, aliliwasilisha pendekezo la kuanzisha medali hiyo baada ya kutazama filamu fupi kumhusu Diagne.
"Imepewa jina la Kapteni Mbaye Diagne kutoka Senegal aliyejitolea maisha yake kuwakoa mamia au pengine raia elfu moja waliokabiliwa na kitisho cha kifo wakati wa mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi na Wahutu wenye msimamo wa wastani miaka 20 iliyopita. Ni shujaa wa Umoja wa Mataifa asiye mfano mwingine na ni heshima kubwa kwetu kuliweka jina lake katika medali hii."
Diagne, ambaye alikuwa miongoni mwa wanajeshi waliohudumu katika kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Rwanda, aliwaokoa Wanyarwanda wengi kwa kuwasaidia kuvuka vituo vya upekuzi vilivyowekwa na wanamgambo wa kihutu, waliokuwa wakifanya mauaji ya kiholela. Aliuwawa alipokuwa kazini mnamo Mei 31 mwaka 1994 akiwa na umri wa miaka 36.
Balozi wa Rwanda amsifu Diagne
Akitoa heshima zake katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, balozi wa Rwanda katika Umoja wa Mataifa, Eugene-Richard Gasana, alitirikwa na machozi mara kadhaa baada ya kushindwa kujizuia hisia za machungu zilipomzidi katika chumba cha mkutano cha baraza la usalama. Alimtaja kapteni Mbaye kuwa shujaa aliyekwenda kinyume na amri za wakuu wake kuyaokoa maisha wakati wa mauaji ya siku 100 ambapo Watutsi walio wachache na Wahutu wenye msimamo wa wastani zaidi ya 500,000 waliuwawa na Wahutu wenye msimamo mkali.
"Alipokabiliwa na uovu, alikataa kuwa mtazamaji," alisema Gasana hapo jana. "Akiwa amejihami tu na ujasiri na hisia ya uwajibikaji kapteni Diagne aliamua kufanya operesheni kadhaa - kuwaokoa mamia, au pengine Wanyarwanda elfu moja," akaongeza kusema Gasana.
Balozi wa Senegal katika Umoja wa Mataifa, Abdou Salam Diallo, alimpongeza Diagne kama "mwana wa kiume mstahiki wa Umoja wa Mataifa, mwanajeshi wa kulinda amani aliyekufa kama shujaa."
Baraza la usalama lenye wanachama 15 limemuomba katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, kuanzisha katika miezi sita ijayo, muundo wa medali hiyo pamoja na kuangalia vigezo vitakavyotumiwa kuwateua na kuwachagua wanajeshi, polisi na wafanyakazi wa kawaida wa umoja huo watakaostahiki kupewa medali hiyo.
Mwandishi: Josephat Charo/AFPE/http://www.unmultimedia.org
Mhariri:Yusuf Saumu