Umoja wa Mataifa waishutumu Rwanda
13 Mei 2016Ripoti ya siri iliyowasilishwa kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa inaituhumu Rwanda kwa kuendelea kuwaunga mkono kimafunzo, kifedha na usaidizi wa kimipango, waasi wa Burundi wanaotaka kumuondoa madarakani, rais wa nchi hiyo, Pierre Nkurunziza.
Jopo lililowahusisha wataalamu sita wa kujitegemea, lililoteuliwa na Umoja kwa Mataifa kufuatilia vikwazo vilivyowekwa na baraza la Usalama la Umoja huo dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, limewasilisha ripoti hiyo ya siri mwezi Februari, inayoeleza kuwa wapiganaji 18 wa Kirundi walioko Mashariki mwa Congo, walikiri kupewa mafunzo na wakufunzi ambao pamoja na wengine ni watumishi wa jeshi la Rwanda, wakiwa kwenye kambi ya wakimbizi nchini Rwanda, katikati ya mwaka 2015, na wataalamu.
Kwenye ripoti hiyo wataalamu, ambayo shirika la habari la Reuters iliiona, na inayotarajiwa kujadiliwa na kamati ya vikwazo ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo, wanasema misaada ya kuwaunga mkono waasi hao kutoka nje imeendelea tangu mapema mwaka 2016.
"Uungwaji mkono huu umekuwepo kwa njia ya mafunzo, ufadhili wa kifedha na usaidizi wa kimipango kwa wapiganaji wa Burundi wanaotoka Rwanda hadi Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo"; imeeleza sehemu ya ripoti hiyo ya wataalamu.
Jopo hilo lilikutana na raia wa Rwanda pamoja na wale wanaodai walihusishwa kwenye mafunzo ya wapiganaji wa Burundi ama wale waliopelekwa DRC ili kuwaunga mkono wapinzani wa Burundi. Ripoti hiyo imesema.
Matokeo ya ripoti hii yanakinzana na mapendekezo yaliyotolewa na maafisa wa Ulaya katika miezi ya hivi karibuni ambao walisema Rwanda ilisitisha kuwaunga mkono kwa namna yoyote waasi wa Burundi tangu jana. Marekani ilionyesha wasiwasi wake kutokana na ripoti kwamba Rwanda inajihusisha na masuala ya ndani ya Burundi.
Rwanda imekana madai hayo
Machafuko ya kisiasa yameendelea kuigubika Burundi kwa kipindi cha mwaka mmoja sasa tangu Nkrunziza alipogombea na kushinda awamu ya tatu ya Urais. Mzozo huo uliibua wasiwasi kwamba unaweza kusababisha machafuko hayo kuwa ya kikabila, kwenye ukanda huo ambao kumbukumbu ya mauaji ya halaiki kwa nchi jirani ya Rwanda ya mwaka 1994 zikiwa bado hazijapotea.
Burundi ina makabila mawili makuu ya Hutu walio wengi na Tutsi walio wachache, na makabila hayo yamesambaa hadi nchi jirani ya Rwanda.
Wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa wamesema wamewasilisha ripoti hiyo ya uchunguzi kwa serikali ya Rwanda ambayo hata hivyo imekana kuhusika kwa namna yoyote, ikisema haikuwa na taarifa zozote za mafunzo yanayotolewa kwa wakimbizi wa Burundi waliokuwa kwenye kambi ya Mahama. Ujumbe wa Umoja wa mataifa uliopo Rwanda haukutaka kuzungumzia chochote kuhusu ripoti hiyo.
Baadhi ya wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wametaka kupelekwa kwa vikosi vya usalama vya umoja huo nchini Burundi ili kukabiliana na machafuko na kusimamia mpaka wa Rwanda na Burundi.
Aidha, ripoti hiyo imeeleza kuwa baadhi ya maafisa wa Kongo wamesema Korea Kaskazini imekuwa ikitoa silaha aina ya bastola kwa majeshi na polisi wa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na polisi, na ilituma wakufunzi kusaidia kutoa mafunzo kwa walinzi wa Rais na vikosi maalumu.
Hali ya kisiasa nchini humo si ya kuridhisha, kutokana na wapinzani wa Rais Joseph kabila kumtuhumu Kabila kwamba anataka kung'ang'ania madaraka baada ya muhula wake kumalizika mwaka 2016. Kabila hajazungumzia chochote kuhusu mategemeo yake ya baadae.
Mwandishi: Lilian Mtono/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef