Umoja wa Mataifa wajadili ajali ya ndege
18 Julai 2014Kikao cha dharura cha harura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichofanyika muda mchache uliopita jijini New York, kilianza kwa wajumbe wote kunyamaza kimya kwa dakika moja kuwakumbuka wale walioangamia katika mkasa huo wa kusikitisha.
Wanachama wa Baraza hilo wametaka wachunguzi wa kimataifa kupewa nafasi ya kuingia eneo la ajali na kufanya uchunguzi huru unaoendana na viwango vya kimataifa.
"Tunaomboleza vifo vya raia wetu 9 waliokuwamo ndani ya ndege hii. Huu ni wakati mgumu kwa jamii ya kimataifa. Hili litahitaji uchunguzi wa kimataifa unaoendana na muongozo wa mamlaka wa usafiri wa anga," alisema Balozi wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa, Mark Lyall Grant
Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Ukraine Arseniy Yatsenyuk ameielezea ajali hiyo kuwa "uhalifu wa kimataifa" ambao walioufanya wanapaswa kuadhibiwa katika mahakama ya kimataifa.
"Huu ni uhalifu dhidi ya binaadamu, kila mtu anapaswa kuwajibishwa, namaanisha kila mtu anayewaunga mkono hawa magaidi ukiwemo utawala wa Urusi," alisema Yatsenyuk.
Familia za walioangamia waelezea masikitiko yao
Kati ya abiria 298 waliokuwamo katika ndege hiyo ni raia 189 kutoka Uholanzi, raia 44 kutoka Malaysia, Wa Australia 27, Waindonesia 12, Raia 9 kutoka Uingereza, wanne kutoka Ujerumani na Ubelgiji, raia watatu kutoka Ufilipino, na mmoja kutoka Canada na New Zealand. Shirika la ndege la Malaysia limesema linaendelea na juhudi za kujua utaifa wa abiria wengine wanne.
Familia za walioangamia wamekusanyika katika uwanja wa ndege wa Kuala Lumpur, na Schiphol Uholanzi wote wakisubiri habari zaidi juu ya kile kilichotokea katika mkasa huo.
Akmar Mohamad Noor, aliye na umri wa miaka 67 kutoka Kuala Lumpur anasema dadake alikuwa anarejea nyumbani kwa mara ya kwanza baada ya miaka mitano kuitembelea familia. Amesema kabla ya kuabiri ndege dadake alimpigia simu na kumuambia wataonana muda mfupi ujao, lakini hilo halikuezekana.
Huku hayo yakiarifiwa Rais wa Urusi Vladimir amesema anawasiliana na mwenzake wa Ukraine Petro Poroshenko na kutoa matumaini kuwa mgogoro wa Ukraine unaoaminika kuchangia pakubwa katika kudeguliwa kwa ndege ya shirika la Malaysia utapatiwa suluhisho.
Lakini kwa upande wake kiongozi wa waasi wanaotaka kujitenga Mashariki mwa Ukraine ameondoa uwezekano wa kufikia msimamo wa pamoja na Ukraine wa kusimamisha mapigano kwa muda lakini akasema watatoa nafasi kwa wachunguzi kuingia eneo ilipoanguka ndege hiyo ya Malaysia.
Mwandishi: Amina AbubakarAP/Reuters/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef