Umoja wa Mataifa wajadili mgogoro wa Sudan
27 Aprili 2012Umoja wa Afrika umelitaka Baraza la Usalama kuidhinisha masharti yake kuwa Sudan hizo mbili zisitishe uhasama wao katika saa 48, zianze mazungumzo katika wiki mbili zijazo, na kuafikiana kuhusu mpango wa amani katika miezi mitatu. Mswada wa Marekani unaunga mkono masharti hayo ya Umoja wa Afrika na unazitaka nchi hizo mbili zisitishe mapigano mara moja na kuvirejesha vikosi vyao katika mipaka yao.
Azimio hilo linasema Baraza la Usalama litatahmini utekelezaji wa masharti hayo ya AU na huenda likachukua hatua zaidi zinazofaa chini ya kifungu cha 41 sura ya saba cha mkataba wa Umoja wa Mataifa, ambacho kinakubali vikwazo na wala siyo nguvu za kijeshi.
Mashambulizi ya anga yakomeshwe
Kuongezeka kwa machafuko katika maeneo ya mpaka wao kumefanya Sudan kushutumiwa kwa kufanya mashambulizi ya angani upande wa Kusini.
Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika lilikutana Jumanne na kuzionya Sudan Kusini na Sudan kuwa litachukua hatua ikiwa hazitasitisha mapigano na kuanza mazungumzo. Aidha lililiomba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuidhinisha azimio hilo chini ya kifungu cha saba cha mkataba wa Umoja wa Mataifa.
Wajumbe hata hivyo wamesema kuwa wanachama kadhaa wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lenye nchi wanachama 15 wana wasiwasi kuhusu vitisho hivyo vya vikwazo.
Balozi wa Marekani katika Umoja huo Susan Rice aliwaambia waandishi wa habari kuwa mazungumzo kuhusu mswada huo yameanza lakini hakutoa maelezo zaidi.
Mazungumzo ya haraka ni muhimu
Rice alisema lengo la rasimu hiyo lilikuwa kuyaunga mkono mapendekezo ya Umoja wa Afrika, katika mfumo ambao Umoja huo ulitaka. Balozi huyo wa Marekani alisema mazungumzo hayo yatachukua siku kadhaa, akiongeza kuwa kwa mtazamo wa Marekani, pamoja na wanachama wengi wa Baraza hilo ni kuwa suala hilo ni la dharura na hivyo linapaswa kushughulikiwa haraka.
Mazungumzo hayo ya Umoja wa Mataifa yaliendelea wakati Mjumbe wa Marekani akidokeza kuwa Sudan na Sudan Kusini zitatoa taarifa hivi karibuni zikitangaza kumalizika kwa mapignao na kufungua milango ya mazungumzo.
Princeton Lyman, mjumbe maalum wa Marekani kuhusu Sudan na Sudan Kusini alisema serikali hizo mbili zitasonga mbele baada ya Jumuiya ya Kiarabu kukutana na kuujadili mzozo huo.
Wakati huo huo shinikizo la kuzitaka nchi hizo mbili kuweka chini silaha linaonekana kufua dafu, baada ya Afisa mmoja wa sudan Kusini kusema kuwa Sudan haikufanya mashambulizi yoyote dhidi ya mipaka yao jana Alhamisi.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Daniel Gakuba