Umoja wa Mataifa waonya kuhusu janga Sudan Kusini
1 Mei 2014Kamishna wa tume ya kutetea haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa Navi Pillay amewashutumu Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir na kiongozi wa waasi Riek Machar kutokana na kutokujali kwao kuhusu hatari ya kuzuka baa la njaa nchini humo na kusema ameshtushwa na mienendo yao.
Matamshi hayo ya Pillay ambaye alikuwa katika ziara ya siku mbili Sudan Kusini, akiandamana na mjumbe maalum wa umoja wa Mataifa kuhusu kuzuia mauaji ya halaiki Adama Dieng, yanakuja baada ya kufanya mazungumzo na viongozi hao wa Sudan Kusini na siku moja baada ya Umoja wa Mataifa kuomba kusitishwa kwa mapigano kwa mwezi mmoja ili kuepusha baa la njaa na janga la kibindamu.
Dieng amewaambia wanahabari kuwa wanawaahidi waathiriwa wa vita vya Sudan Kusini kuwa watafanya kila wawezalo kuepusha mauaji ya halaiki kama yaliyotokea Rwanda na kwamba hakuna sababu ya kutochukua hatua zifaazo kuepusha janga hilo.
Mzozo wa Sudan Kusini umechukua mkondo hatari
Maafisa hao wakuu wa Umoja wa Mataifa wamesema ni bayana kuwa mzozo huo umechukua mkondo hatari ambapo raia wanalengwa kimakusudi kwa misingi ya makabila yao.Mzozo huo wa Sudan Kusini umesababisha vifo vya maelfu ya watu na kuwaacha takriban watu milioni moja na laki mbili bila makaazi.
Pillay amesema kiasi ya watoto elfu tisa wamesajiliwa kuwa wapiganaji na pande zote mbili katika mzozo huo na kuwashutumu viongozi wa nchi hiyo kuwa badala ya kulijenga taifa lao wanashughulika tu na maslahi ya kibinafsi ya kujitakia madaraka.
Shirika la kushughulikia maslahi ya watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF limeonya kuwa kiasi ya watoto elfu hamsini huenda wakafariki kutokana na utapia mlo mwaka huu huku watu milioni saba wakiwa katika hatari ya kukabiliwa na njaa kufuatia uhaba wa chakula.
Baa la njaa kuwaathiri watu milioni moja
Watu wengi hawajaweza kupanda mashamba yao katika msimu huu wa kilimo baada ya kutoroka makwao na hivyo kuiweka Sudan Kusini katika hatari ya kukosa mavuno.
Shirika la mpango wa chakula duniani WFP limesema lina nakisi ya dola milioni 224 zinazohitajika kuwalisha zaidi ya watu milioni moja na kwamba nchi nyingi zilizoahidi kutoa msaada hazijafanya hivyo.Mkutano wa wafadhili kuchangisha fedha za kuisadia Sudan Kusini umepangwa kufanyika tarehe 20 mwezi huu.
Huku Pillay na Dieng wakikamilisha ziara yao,waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Marekani John Kerry aliwasili Ethiopia hapo jana na anatarajiwa kuzishurutisha pande hizo mbili kumaliza vita hivyo kwa kufanya mazungumzo na wajumbe na wapatanishi katika mazungumzo ya kutafuta amani Sudan Kusini, ambayo yanafanyika mjini Addis Ababa na pia anatarajiwa kuzuru Juba wakati wa ziara yake.
Kerry amesema serikali ya Marekani inazingatia kuwawekea vikwazo viongozi wa Sudan kusini ambao amesema wanazingatia tu kujitajirisha kupitia uuzaji wa mafuta na kujipatia madaraka.
Mwandishi:Caro Robi/ap/afp
Mhariri: Daniel Gakuba