1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa waonya kuhusu mgogoro wa jimbo la Kasai

5 Julai 2018

Watalaamu wa Umoja wa Mataifa wameonya kwamba mgogoro katika jimbo la Kasai nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo unaweza kuwa mwanzo wa mauaji ya kimbari.

https://p.dw.com/p/30sMg
Türkei Polizeigewalt Human Rights Watch
Picha: Getty Images/A.Altan

Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa anayechunguza mateso Nils Melzer  aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba kuwaua watu kwa kuwakatakata viungo, ubakaji wa makundi na mauaji ni visa ambavyo vimenakiliwa katika jimbo la Kasai nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na matukio haya yanaweza kuwa ni msingi wa mauaji ya kimbari.

Mchunguzi huyo ametoa wito wa kuchukuliwa hatua ili kuzuia mauaji mengine ya halaiki kama yale yaliyotokea huko nchini Rwanda au Srebrenica. Bwana Melzer, mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa anayechunguza mateso duniani kote, amesema ameshtushwa na ripoti iliyotolewa na watalaamu wa shirika la kutetea haki za binadamu la Umoja wa Mataifa ambayo alitaja kwamba waasi na majeshi ya serikali ya Kongo walifanya uhalifu wa kibinadamu ikiwa ni pamoja na ubakaji wa makundi yaani watu wengi kumbaka mtu mmoja kwa wakati mmoja, kuwala watu na kuiharibu miili ya watu baada ya kuwaua.

Nembo ya Shirika la Umoja wa Mataifa la kutetea haki za binadamu
Nembo ya Shirika la Umoja wa Mataifa la kutetea haki za binadamuPicha: Getty Images/AFP/J. Macdougall

Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa imejikita kwenye ripoti ya awali iliyozilaumu pande zote kwa kutenda uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu iliyogusia mashambulizi ya kikatili wakati wa vita vya eneo la kati la Kasai.

Jeshi la Kongo lilishirikiana na waasi wa Bana Mura liliwapinga wanamgambo wa Kamuina Nsapu katika vita vya kikabila ambavyo vilianza mnamo mwaka 2016 na bado vinatokota chini kwa chini hadi sasa. Vita hivyo vilikuwa moja ya mfululizo wa mapigano yaliyotokea nchini Kongo wakati rais Joseph Kabila alipokataa kuondoka madarakani muda wake ulipomalizika mwishoni mwa mwaka 2016.

Kina mama wa Kasai  na watoto wao
Kina mama wa Kasai na watoto waoPicha: picture-alliance/dpa/K. Bartlett

Mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994 yalisababisha Watutsi na Wahutu wenye msimamo wa wastani wapatao 800,000 kuuawa katika muda wa siku 100. Mauaji hayo yalitekelezwa na serikali iliyokuwa inayoongozwa na Wahutu kwa ushirikiano na wapiganaji wa kikabila. Umoja wa Mataifa na nchi zenye nguvu zilishindwa kuzuia mauaji hayo licha ya kupokea taarifa za mapema.

Na huko Srebrenica wanaume na wavulana wapatao 8,000 wa Kiislamu waliuawa katika mauaji yaliyofanywa na askari wa Bosnia wenye asili ya Kiserb kwa amri ya jenerali wa zamani Ratko Mladic. Umoja wa mataifa uliandaa sehemu salama mnamo mwezi Julai mwaka1995. Mauaji hayo ndio makubwa zaidi kutokea barani Ulaya tangu kumalizika vita kuu vya pili vya dunia.

Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa anayechunguza mateso Nils Melzer  ambaye pia ni mwanasheria wa kimataifa amesema kwa sasa jimbo la Kasai ni Jahannamu inayosubiri kulipuka.

Mwandishi: Zainab Aziz/RTRE

Mhariri: Iddi Ssessanga