1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa wataka uchuguzi mauwaji Gaza

18 Mei 2018

Afisa wa ngazi ya juu kabisa mwenye jukumu la kusimamia masuala ya haki za binaadamu katika Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad al-Hussein amesema kuna ushahidi mdogo unaonesha kuwa Israeli ilifanya jitihada za kupunguza maafa,

https://p.dw.com/p/2xxrr
UN-Hochkommissar Menschenrechte Said Raad al-Hussein
Picha: picture-alliance/Keystone/M. Trezzini

Kamishina Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la haki za binadamu, Zeid Ra'ad al-Hussein aliyasema hayo katika kikao maalum cha baraza la haki za binaadamu la Umoja wa Mataifa, kufuatia kile kinachoitwa ukandamizaji wa mauwaji, waliofanyiwa waandamanaji na majeshi ya Israel mjini Gaza. Vikosi vya Israel vililishambulia eneo la Gaza lililo chini ya utawala wa Hamas na kusababisha vifo vya karibu Wapalestina 60, katika maandamano yaliojumisha idadi kubwa ya watu kwenye eneo la mpakani Jumatatu.

Uchunguzi wa kimataifa ni muhimu

Drohnen und Drachen überfliegen Gaza-Proteste
Waandamanaji katika eneo la mpakani la Ukanda wa GazaPicha: Reuters/I.A. Mustafa

Kikao hiki cha leo kitazingatia azimio lililotolewa na Pakistan na matiafa mengine ya Kiislamu, linalojumisha wito wa kuundwa kamisheni huru ya kimataifa ya kuchunguza mauwaji hayo. Zeid amenukuliwa akisema kuna ushahidi finyu wenye kuonesha kulikuwepo na jitihada za kupunguza maafa yaliotokea katika maandamano hayo.

Amesema waandamanaji walitumia aina fulani vya viripuzi visivyo na madhara makubwa, mikasi ya kukatia seng'eng'e katika uzio wa mpakani ambavyo vyote kwa ujumla wake haviwezi kutishia maisha au kusababisha majeraha yenye kusababisha hatari ya kifo, mambo ambayo hayawezi kutoa uhalali kwa jeshi la Israel kutumia silaha za moto.

Aidha, aliongeza kusema kuwa tangu Machi 30, mwaka huu vikosi vya Israel vimewauwa Wapalestia 106, wakiwemo watoto 15. Zaidi ya watu wengine 12,000 wamejeruhiwa, miongoni mwa hao 3,500 kwa risasi.

Israel na Marekani zatoa tuhuma

Israel na Marekani zilirejea tena kuwatuhumu wajumbe 47 wa baraza hilo kuwa ni wapinzani wa Israel na wanajiegemeza upande mmoja. Katika kikao hicho Balozi wa Israel Aviva Raz Schechter, amesema wito huo wa kuundwa kwa kamisheni ya uchunguzi ni jambo la kisiasa na kwamba halitaweza kupunguza hali ya fukuto la vurugu katika eneo maeneo ya machafuko. Kwa ujumla Israel imejitetea kuwa mauwaji yaliyotokea katika maandamano yalipangwa na kundi la Hamas, kundi la wanamgambo lenye kuidhibiti Gaza.

Takribani watu milioni mbili wanaisha katika eneo la Ukanda wa Gaza, wengi wa watu hao ni wasio na mataifa. Wakazi katika eneo hilo waliliambia shirika la habari la Uingereza, Reuters kwamba Israel inastahili kukosolewa kimatifa kutokana na mkasa wa Jumatatu.

Mwandishi; Sudi Mnette/APE
Mhariri: Grace Patricia Kabogo