Umoja wa Mataifa wataka uchunguzi huru mauaji ya Khashoggi
16 Desemba 2018"Kwa kweli ni jambo la muhimu sana kuwa na uchunguzi wa maana na kuwaadhibu wale waliohusika na mauaji nhaya," alisema Guterres kwenye mkutano mjini Doha, Qatar.
Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alisema hakuwa na taarifa juu ya mkasa huo zaidi ya zile anazozipata kupitia vyombo vya habari.
Khashoggi, raia wa Saudi Arabia aliyekuwa mchangiaji wa makala kwenye jarida la Washington Post, aliuawa tarehe 2 Oktoba muda mfupi baada ya kuingia kwenye jengo la ubalozi mdogo wa nchi yake mjini Istanbul, Uturuki, katika kile ambacho serikali ya nchi yake inachokiita kuwa ni "operesheni iliyokwenda kombo."
Mara kadhaa, Saudi Arabia imekataa matakwa ya Uturuki ya kuwapeleka washukiwa wa mauaji hayo nchini Uturuki kukabiliana na mkono wa sheria.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu, alisema kwenye kongamano hilo la Qatar kwamba nchi yake kamwe isingevunjika moyo na kuubaini ukweli kuhusu mauaji hayo.
"Hatujapokea taarifa yoyote mpya au matokeo ya uchunguzi kutoka upande wa Saudia," alisema waziri huyo wa mambo ya nje, akiongeza kwamba "Uturuki kamwe haitaliachia hili, tutakwenda nalo hadi mwisho wake."
Uchunguzi wa kimataifa
Mapema mwezi huu, waziri huyo alisema kuwa Uturuki ilikuwa inazungumza na Umoja wa Mataifa kuhusiana na uchunguzi juu ya mauaji hayo ambayo yamepelekea ukosoaji mkubwa duniani dhidi ya Saudi Arabia.
Kwa mujibu wa Uturuki, kikosi cha watu 15 raia wa Saudi Arabia kilitumwa mjini Istanbul kumuua Khashoggi, mshirika mkuu wa kasri la kifalme aliyegeuka kuwa mkosoaji wa utawala wa mrithi wa kiti cha ufalme, Mohammed Bin Salman.
Tangu kubainika kwa mauaji hayo, serikali ya Saudia inasema imewatia nguvuni washukiwa 21, huku mwanasheria mkuu wa nchi hiyo akitaka watano kati yao wahukumiwe kifo.
Licha ya shutuma kali kwamba Bin Salman aliamuru mauaji hayo binafsi, ufalme wa Saudia umekuwa ukikanusha vikali madai hayo.
Hata hivyo, mauaji hayo yameiathiri vibaya taswira ya kimataifa ya utawala mjini Riyadh, na mataifa ya Magharibi - zikiwemo Marekani, Ufaransa na Canada - yameweka vikwazo wa raia takribani 20 wa Saudi Arabia wanaoshukiwa kuhusika na mauaji hayo.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Zainab Aziz