1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa watakiwa kuweka vikwazo Myanmar

12 Februari 2021

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetakiwa kufikiria kuweka vikwazo vikali vikiwemo vya silaha na marufuku ya kusafiri kwa maafisa wa kijeshi waliofanya mapinduzi nchini Myanmar.

https://p.dw.com/p/3pHgP
Myanmar Min Aung Hlaing
Picha: Tatmadaw True Information Team Facebook page via AP/picture alliance

Akizungumza siku ya Ijumaa katika Baraza la Haki za Binaadamu mjini Geneva, afisa wa Umoja wa Mataifa anayechunguza hali ya haki za binaadam nchini Myanmar, Thomas Andrews amesema kuna ripoti zinazoendelea kutolewa pamoja na ushahidi wa video unaoonesha kwamba vikosi vya usalama vya Myanmar vimetumia risasi za moto dhidi ya waandamanaji tangu jeshi lichukue madaraka takriban wiki mbili zilizopita.

''Mheshimiwa Rais, ninalisihi baraza hili, Umoja wa Mataifa na nchi zote wanachama kuweka angalau masharti manne kwa utawala wa kijeshi wa Myanmar: kwamba wawaachie huru bila masharti yoyote wote waliokamatwa, waache kuwatesa na kuwashtaki watu wa Myanmar kwa kutumia haki zao za msingi, na waachie madaraka haraka, ili serikali ya Myanmar iliyochaguliwa kihalali ianze kazi yake,'' alisisitiza Andrews.

Marekani imeshaweka vikwazo

Marekani ambayo tayari imeiwekea vikwazo Myanmar siku ya Alhamisi, imezitaka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kufuata nyayo zake.

Baraza hilo limeelezea wasiwasi wake kuhusu vikwazo kuwekwa kutokana na mapinduzi ya kijeshi ya Februari Mosi, likisisitiza kuwa linahitaji kuwa mwangalifu hasa kwa ''wanaolengwa'' ili kuepuka kuwadhuru watu wanaoishi katika mazingira magumu.

Naibu kamishna wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayofuatilia haki za binaadamu, Nada al-Nashif ameliambia Baraza la Haki za Binaadamu kwamba ulimwengu unaangalia.

Myanmar Protest Maung Sun
Waandamanaji wa Yangon wanaotaka kuachiliwa huru viongozi waliokamatwa MyanmarPicha: Maung Sun

Chombo hicho cha juu cha Umoja wa Mataifa kilikuwa kinafanya kikao maalum cha dharura kilichoitishwa mwanzoni mwa wiki hii na Uingereza pamoja na Umoja wa Ulaya kuzungumzia mapinduzi ya Myanmar na matokeo yake.

Ama kwa upande mwingine, kiasi ya wabunge 300 wa Myanmar siku ya Ijumaa wameutaka Umoja wa Mataifa kuchunguza ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu, ikiwemo kuwakamata viongozi wa kiraia na kuwapiga risasi waandamanaji, unaofanywa na viongozi wa kijeshi tangu walipochukua madaraka.

Katika barua yao iliyosomwa kwenye Baraza la Haki za Binaadamu na Balozi wa Uingereza Julian Braithwaite, wabunge hao wamesema utawala wa kijeshi umezuia uhuru wa kujieleza kwa kuandaa muswada wa mawasiliano ya simu unaokusudiwa kudhibiti upatikanaji wa mtandao wa intaneti na huduma ya simu za mkononi.

Jeshi lawataka wananchi kutoa ushirikiano

Wakati huo huo, kiongozi wa mapinduzi ya kijeshi ya Myanmar, Jenerali Min Aung Hlaing ametumia fursa ya maadhimisho ya Siku ya Muungano inayoadhimishwa Ijumaa kuwataka wananchi wa taifa hilo kushirikiana pamoja na jeshi iwapo wanataka demokrasia.

Hata hivyo, wito huo unategemewa kukabiliwa na upinzani mkali wa waandamanaji wanaoshinikiza kuachiliwa huru viongozi wanaoshikiliwa ambao walichaguliwa na wananchi, akiwemo Aung San Suu Kyi na zaidi ya watu 350 wakiwemo maafisa, wanaharakati, waandishi habari na wanafunzi.

Soma zaidiUmoja wa Mataifa wataka Suu Kyi kuachiwa huru

Jenerali Hlaing amewataka wananchi wote kuliunga mkono jeshi akisema matukio ya kihistoria yamewapa funzo kwamba ushirikiano wa kitaifa tu ndiyo unaweza kuhakikisha umoja usiovunjika na wenye kuhifadhi mamlaka ya uhuru.

(AP, DPA, AFP, Reuters)