UN yatoa tahadhari ya njaa Haiti, Sahel na sudan
29 Mei 2023Taarifa ya pamoja iliyotolewa Jumatatu na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO imeeleza kuwa mataifa ya Haiti, Burkina Faso, Sudan na Mali yanaungana na Afghanistan, Nigeria, Somalia, Sudan Kusini na Yemen ambayo yako katika viwango vya juu vya tahadhari, pamoja na jamii zinazokabiliwa na kitisho kikubwa cha njaa, kuelekea hali ya janga.
Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Qu Dongyu amesema baa la njaa Sudan linatokana na kuzuka kwa vita, kwenye nchi za Burkina Faso na Mali ni kutokana na vizuizi vikali vilivyowekwa dhidi ya watu kutembea na kusafirisha bidhaa, na nchini Haiti kutokana na mzozo wa kiusalama.
FAO yataka maisha ya watu yaokolewe
Qu ametoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka katika sekta ya kilimo na kuwaokoa watu kutoka kwenye ukingo wa njaa, kuwasaidia kuyajenga upya maisha yao na kutoa suluhisho la muda mrefu kushughulikia sababu kuu za uhaba wa chakula, ili kuokoa maisha na ajira.
Mkurugenzi wa WFP kanda ya Afrika Mashariki, Michael Dunford anasema wasiwasi wake mkubwa ni athari ambazo mzozo wa Sudan utakuwa nazo katika kanda nzima, hususan Sudan Kusini.
''Hata kabla ya huu mzozo, asilimia 70 ya wananchi wa Sudan walikuwa wanahitaji msaada wa kiutu na kwa sasa WFP haiwezi kukidhi mahitaji yao. Tunajitahidi kukidhi mahitaji yoyote yaliyoongezeka katika hatua hii,'' alifafanua Dunford.
Hadi sasa WFP imetoa msaada wa chakula na lishe kwa zaidi ya watu 600,000 walio katika mazingira magumu nchini Sudan.
Ripoti za FAO na WFP zimeeleza kuwa mbali na nchi hizo tisa, mataifa mengine 22 yametambuliwa kama maeneo yaliyo katika hatari ya kukabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.
Hutua zichukuliwe kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi
Mkurugeni Mtendaji wa WFP, Cindy McCain ameonya kuhusu madhara ya janga iwapo hatua za wazi hazitochukuliwa kuwasaidia watu kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na hatimaye kuzuia njaa.
Kwa mujibu wa McCain, sio tu kwamba watu wengi zaidi katika maeneo mengi ulimwenguni wana njaa, lakini ukali wa njaa unaowakabili ni mbaya zaidi kuliko hapo awali.
Aidha, ripoti hiyo imeelezea uwezekano wa mzozo wa Sudan kusambaa, hali itakayozidisha mizozo ya kiuchumi katika nchi masikini na kuongezeka kwa hofu kwamba mvua za El Nino katikati ya mwaka 2023 zinaweza kusababisha hali mbaya ya hewa kwenye nchi zilizo hatarini.
(AP, AFP)