1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa wautanzua mgogoro wa benki kuu ya Libya

Josephat Charo
3 Septemba 2024

Tume ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Libya imeandaa mazungumzo kwa lengo la kuutafutia ufumbuzi mgogoro kuhusu benki kuu ya Libya.

https://p.dw.com/p/4kCYc
Mkuu wa tume ya Umoja wa Mataifa nchini Libya, UNSMIL, Stephanie Williams
Mkuu wa tume ya Umoja wa Mataifa nchini Libya, UNSMIL, Stephanie Williams Picha: Martial Trezzini/KEYSTONE/picture alliance

Tume maalumu ya Umoja wa Mataifa nchini Libya UNSMIL imesema imeongoza mazungumzo mjini Tripoli na wajumbe wa baraza la wawakilishi la Libya, baraza la juu la dola na baraza la rais katika juhudi ya kuutafutia ufumbuzi mkwamo uliopo kati ya makundi mawili hasimu kuhusu udhibiti na usimamizi wa beki kuu na mapato yanayotokana na mauzo ya mafuta.

Mkwamo huo ulitokea wakati makundi kutoka eneo la magharibi yalipochukua hatua ya kumuondoa madarakani gavana mkongwe Sadiq al-Kabir na nafasi yake kujazwa na bodi hasimu, hatua iliyosababisha makundi ya mashariki kusimamisha uzalishaji mafuta.

Taarifa ya UNSMIL imesema mazungumzo yamekamilika kwa maelewano. Wawakilishi wa baraza la wawakilishi la Libya, baraza la juu la dola na baraza la rais wameshiriki mazungumzo hayo yaliyoanza asubuhi hadi usiku jana Jumatatu.