Umoja wa Mataifa yasema kundi la IS lingali kitisho
11 Agosti 2017Kundi linalojiita Dola la Kiislamu linaendelea kuhimiza na kuwezesha mashambulizi duniani kando na kutoa misaada ya kifedha kwa wafuasi wao. Hiyo ni licha ya mashambulizi dhidi ya ngome zake nchini Syria na Iraq. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa.
Ripoti hiyo ya kurasa 24 na ambayo iliandaliwa na jopo la wataalamu kwa niaba ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limegundua viwango vidogovidogo vya fedha zinazotumwa katika mataifa mengine, na huwa vigumu kugundua fedha hizo. Ripoti hiyo inajiri wakati kundi hilo linalojiita Dola la Kiislamu-IS likiimarisha juhudi zake za mashambulizi kimataifa kama ambavyo imeshuhudiwa barani Ulaya.
Fedha wanazotoa kama ufadhili, zinatokana pakubwa na faida za mafuta na kodi wanazotoa watu katika maeneo ambayo bado IS inadhibiti.
IS yataka kujipenyeza Asia
Ikitaja mapigano ya Kusini mwa Ufilipino ambapo watu 700 waliuawa katika kipindi cha zaidi ya miezi miwili, ripoti hiyo imesema kuwa, kando na bara Ulaya, IS inajaribu pia kupenyeza udhibiti wake Kusini Mashariki mwa Asia.
Ripoti imeendelea kudokeza kuwa idadi ya wapiganaji wa kigeni wanaosafiri kuelekea Syria na Iraq imeendelea kupungua. Kadhalika uwezo wake kifedha pia umezidi kudidimia kutokana na operesheni za kijeshi dhidi yake.
Hata hivyo mpango maalum unapaswa kuelekezwa kwa watoto wanaorejea nyumbani huku wamepandikizwa misimamo mikali ya Kiislamu hasa baada ya kupewa mafunzo IS. Ripoti inatilia mkazo kuwa kundi la watoto hao linapaswa kupewa kipaembele na mikakati inayolenga kuwapa ulinzi wa kisheria uwekwe.
Kiungo kikuu kinachotoa mwongozo hakijaporomoka
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, upinzani mkali uliotolewa na IS katika mji wa Mosul ambao serikali ilitangaza kuwa imeukomboa mwezi Julai, ulionesha kuwa kiungo kikuu kinachotoa mwongozo kwa IS hakijavunjika kikamilifu, na hivyo kinasalia kuwa kitisho kikuu cha kijeshi.
Zaidi ya hayo ni kuwa IS imejifunza namna ya kuboresha ndege zinazoendeshwa bila rubani na pia kuunda zao wenyewe kwa ajili ya kufanya ukachero na mashambulizi ya mabomu.
Kwa upande mwingine, kundi la wajihadi la mtandao wa Al-Qaeda bado linadhibiti maeneo kadhaa katika Magharibi mwa Afrika, Mashariki mwa Afrika na rasi ya Arabia hususan Yemen huku likiruhusu wapiganaji kati ya makundi hayo mawili yenye ushindani kutoka katika kundi moja na kujiunga na jingine.
Afrika Mashariki inakumbwa na kitisho cha mashambulizi kutoka kwa kundi la Al-Shabaab ambalo lina mshikamano na mtandao wa Al-Qaeda ulio na wapiganaji kati ya 6000 hadi 9000.
Nchini Afghanistan ripoti hiyo inasema kuwa IS imeimarisha ushindani wake dhidi ya Taliban na inalenga kujipanua japo haijaunda kundi la wapiganaji katika eneo hilo.
Jopo la wataalamu walioandaa ripoti hiyo limelitaka Baraza la Usalama kuzikumbusha nchi wanachama wake kuwa kulipa fidia ili kuwakomboa wanaoshikwa mateka ni kinyume cha sheria kwa mtizamo wa vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya makundi hayo.
Mwandishi: John Juma/ APE/AFPE
Mhariri: Mohammed Khelef