EU, NATO kuipa msaada Uturuki
10 Machi 2020Tumo katika mkanganyiko, amesema rais wa halmashauri ya Umoja bwa Ulaya Ursula von der Leyen baada ya kukutana na Erdogan mjini Brussels jana, lakini makubaliano kuhusu wakimbizi yataendelea.
Hali katika jimbo la Idlib ni kitisho kwa Ulaya yote, amesema rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alipokutana na katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg. na hakuna mtu anaweza kuangalia kwa njia nyingine mzozo wa kiutu katika eneo hilo. Uturuki imefanya vya kutosha kuliko nchi nyingine mwanachama wa NATO, ndio sababu nchi hiyo inatarajia mshikamano.
Recep tayyip Erdogan akiwa mwenye kujiamini alikutana na wawakilishi wa NATO , ambao walizungumzia kuhusu kufanya tafakuri juu ya kutoa msaada kwa Uturuki. Wakati huo huo lakini wawakilishi hao wa NATO waliitaka Uturuki kutafuta suluhisho la muda mrefu katika Syria , na kumkumbusha rais Erdogan , kwamba kwa hatua yake ya kununua mfumo wa kukinga makombora kutoka Urusi amejikuta bila marafiki. Akizungumza katika mkutano na waandishi habari pamoja na rais wa Uturuki, Recep Erdogan, katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg alisema:
"Hakuna mshirika wetu mwingine yeyote aliyeathirika zaidi na mashambulizi ya kigaidi, na hakuna mshirika anayewahifadhi wakimbizi wengi zaidi. NATO itaendelea kuiunga mkono Uturuki kwa hatua kadhaa tofauti."
Kwa upande wa Umoja wa Ulaya unabaki katika dhamira yake katika mkataba wa wakimbizi na makubaliano hayo yataendelea kuwa hai, rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen alisema jana jioni baada ya kukutana na rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan mjini Brussels. Mazungumzo hayo yalifanyika baada ya mvutano wa siku kadhaa kati ya Umoja wa Ulaya na Uturuki kuhusiana na suala la wahamiaji katika mpaka kati ya Uturuki na Ugiriki. Rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen akizungumza katika mkutano na waandishi habari amesisitiza kuhusu msaada kwa Uturuki.
"Wahamiaji wanahitaji msaada, Ugiriki inahitaji msaada, lakini pia Uturuki inahitaji kuungwa mkono , na hii inahusu kupatikana njia kuelekea mbele pamoja na Uturuki. Bila shaka tuna tofauti zetu lakini tumezungumza wazi juu ya haya na yalikuwa mazungumzo mazuri, yalikuwa majadiliano mazuri na yalikuwa yenye manufaa."
Von der Leyen amesema kuwa tathmini itafanyika kuhusu sehemu gani ya makubaliano haijatekelezwa na kwa nini. Pia akizungumza baada ya mkutano huo , rais wa baraza la Ulaya Charles Michel amesema mkuu wa sera za mambo ya kigeni wa Umoja huo na waziri wa mambo ya kigeni wa Uturuki wanapaswa kufanyakazi kwa pamoja na timu ya wataalamu na kutoa ufafanuzi wa tofauti za mawazo zilizopo katika utekelezaji wa makubaliano katika muda wa siku chache zijazo.