1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya na nchi za ACP karibu kufikia makubaliano

Mohamed Dahman8 Machi 2007

Halmashauri ya Umoja wa Ulaya na kundi la nchi kutoka Afrika,Carribean na Pasifiki ziko karibu kufikia makubaliano juu ya uregezaji wa masharti ya biashara kufuatia juhudi zao za karibuni kabisa katika mazungumzo mazito na magumu.

https://p.dw.com/p/CHlW
Nchi za Afrika na Caribbian zinataka kuziuza bidhaa zao barani Ulaya
Nchi za Afrika na Caribbian zinataka kuziuza bidhaa zao barani UlayaPicha: PA/dpa

Kamishna wa biashara wa Umoja wa Ulaya Peter Mandelson amekazania tishio la Umoja wa Ulaya katika mkutano wa wiki iliopita kamba nchi za Kiafrika,Carribean na Pasifiki ACP zitapoteza nafasi yao ya upendeleo kwa masoko ya Umoja wa Ulaya iwapo Makubaliano ya Ushirikiano wa Kiuchumi hayatotiwa saini ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Huo ni muda wa mwisho uliotolewa na Shirika la Biashara Duniani WTO wa kumalizika kwa msahama wa kuendeleza ushuru wa upendeleo uliopo hivi sasa chini ya makubaliano yaliotiwa saini kati ya Umoja wa Ulaya na nchi za ACP mjini Cotonou katika taifa la Afrika Magharibi la Benin hapo mwaka 2000.

Nchi za ACP zimeiomba Halmashauri ya Umoja wa Ulaya ambayo ni kitengo kikuu cha utendaji cha umoja huo kuhakikisha kwamba mtiririko wa biashara hautoathiriwa baada ya mwaka 2007.

Katika mkutano wa wiki iliopita nchi hizo na halmashauri hiyo zimekubaliana kuendeleza jitihada za kutekeleza hatua za maandalizi kukamilisha mazungumzo kwa msaada na Umoja wa Ulaya bila ya kujifunga kwa muda wa kumaliza mazungumzo hayo.Mkutano huo umeshindwa kutowa maafikiano ya pamoja.

Nchi 79 za ACP kutoka katika kanda sita Caribbean kanda nne za Afrika na Pasifiki inaonekana kugawika juu ya dharura ya kufikia makubaliano.

Gilles G. Hounkpatin mwakilishi wa biashara wa Jumuiya ya Kichumi ya mataifa ya Afrika Magharibi ECOWAS amesema kipau umbele chao ni makubaliano yanayokidhi maslahi yao.

Kwa upande mwengine nchi za Carribean zinasema ziko tayari kusaini makubaliano makubwa ya biashara.Mjumbe wa Carribean Junior Lodge anasema Carribean inasisitiza kufikiwa kwa makubaliano kamili katika muda mfupi kadri inavyowezekana kwa sababu wana mtaji mdogo sana wa kuzungumza na nafasi katika masoko ni kitu pekee wanachoweza kutowa na badala yake wanataka wafaidike kwa kadri inavyowezekana.Mjumbe huyo anaamini Ulaya ina utashi wa kuvamia masoko katika kufunguwa masoko ya nchi za ACP kwa bidhaa zake za kilimo.

Mariano Iossa kutoka shirika la Actionaid ana maoni kama hayo kwamba Ulaya inapoteza uwezo wake wa ushindani katika masoko ya nchi zinazoinukia kiuchumi kwamba zinataka kuwa mbele ya China hasa katika kufunguwa masoko ya huduma za fedha katika nchi zenye utajiri wa mafuta na rasimali.

Kanda zote za ACP zimekubaiana juu ya haja ya kuwepo kwa muda wa mpito wa hadi miaka 25 kwa ajili ya kufunguwa masoko yao kwa bidhaa za Ulaya na hatua ya kuchukuwa moja kwa moja dhidi ya kufurika kusikotegemewa kwa bidhaa kutoka Ulaya. Pia zinataka kujuwa vipi halmashauri hiyo ya Umoja wa Ulaya itakavyotumia euro bilioni 2 ilizoahidi kuufanya uchumi wa nchi za ACP kuwa wa ushindani zaidi.

Mashirika ya maendeleo yasio ya kiserikali ya Ulaya yameupachika jina mkakati wa majadiliano wa Umoja wa Ulaya kuwa ni wa usaliti.

Umoja wa Ulaya unaendelea kushikilia hoja yake kwamba makubaliano ya Ushirikiano wa Kiuchumi ni bora zaidi kuliko ya Cotonou.