1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hakutakuwa na ugumu katika suala la mipaka ya Ireland

Admin.WagnerD8 Desemba 2017

Mazungumzo ya Uingereza kujitoa katika Umoja Ulaya, yanatoa mwelekeo wa  kuingia  awamu ya pili ya mazungumzo hayo kuhusu ushirikiano wa kibiashara baina ya pande hizo mbili. 

https://p.dw.com/p/2p0Jq
Belgien May und Juncker in Brüssel
Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May na Rais wa EU Jean-Claude Juncker wakizungumza na wanahabari. Desemba 8, 2017.Picha: Getty Images/AFP/E. Dunand

Mazungumzo hayo ya Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya, yameonyesha njia  kwa pande hizo mbili kuendelea mbele katika hatua ya majadiliano inayofuata. Mwenyekiti wa halmashauri Kuu ya umoja wa Ulaya, Jea Claude Juncker, ameyasema hayo leo.

Mtendaji huyo wa Umoja wa Ulaya ; amesema  makubaliano yamefikiwa baada ya mazungumzo mazito ambayo yataruhusu kupanuka zaidi kwa mazungumzo hayo, ikiwamo mustakabali wa uhusiano wa kibiashara  na kipindi cha mpito.

 Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Donald Tusk, aliwaambia wanahabari kuwa majadiliano ya kina kuhusu mustakabali wa uhusiano katika maeneo ya mazingira, ulinzi na usalama, yanaweza sasa kuanza.

 Alisistiza kuwa licha ya makubaliano hayo kufikiwa, changamoto kubwa bado inawakabili mbele yao.

``Katika kipindi hiki cha mpito ninashauri kwamba Uingereza iheshimu sheria zote za Umoja wa Ulaya ikiwamo sheria mpya. Itaheshimu maazimio ya kibajeti na sheria za nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya na majukumu yote yanayohusiana``amesema Tusk.

Belgium Fahnen Großbritannien und EU
Bendera ya Uingereza na ya Umoja wa Ulaya.Picha: picture alliance/AP Photo/V. Mayo

 Tusk awatumia miongozo viongozi wa EU 

Kadhalika Tusk amesema amewatumia miongozo viongozi wa Umoja wa Ulaya kuhusu namna anavyofikiri  mazungumzo ya Brexit yanaweza kufanyika baada ya Uingereza, Ireland na maofisa wa Umoja wa Ulaya kufikia maamuzi hayo leo.

Hata hivyo, haitashiriki katika kufanya maamuzi yatakayofanywa na nchi 27 zilizobaki wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Umoja wa Ulaya, umekuwa ukihimiza uwazi katika  masuala matatu , mpaka wa Ireland, makubaliano ya kifedha na haki za raia wa Umoja wa Ulaya,nchini Uingereza, kabla haijakubali kuanza awamu ya pili ya  mazungumzo ya   Brexit.

``Haya ni majadiliano magumu lakini tumeshapiga hatua kubwa. Nimeridhika na mipango ya haki tuliyoifikia na Uingereza.`` Amesema Juncker

  Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May amesema makubaliano baina ya Uingereza na Umoja wa Ulaya yamejihakikishia haki ya raia  milioni tatu wa Umoja wa Ulaya wanaoishi Uingereza na raia wa Uingereza milioni 1 wanaoishi katika nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya.

 Kadhalika amesema majadiliano hayo  yamehakikisha kuwa hakutakuwa na ugumu wa kuvuka mipaka kati ya Ireland ya Kaskazini na Jamhuri ya  Ireland baada ya mazungumzo hayo ya Brexit.

Awali kabla ya mazungumzo hayo,  May aliwasili Brussel mapema leo asubuhi na kukutana na Jean Claude Juncker baada yajuhudi kadhaa za usiku kucha kuonekana kufanikisha kufikiwa makubaliano  katika suala la mpaka wa Ireland.

Mwandishi: Florence Majani

Mhariri: Saumu Yusuf