Umoja wa Ulaya una msimamo wa pamoja kuhusu Brexit
27 Aprili 2017Hayo yamesemwa leo(27.04.2017) na kansela Merkel bungeni wakati akilihutubia bunge kabla ya mkutano wa viongozi wa mataifa 27 yaliyobakia katika Umoja huo mjini Brussels siku ya Jumamosi.
Mataifa 27 ya Umoja wa Ulaya yanaingia katika mchakato wa miaka miwili wa majadiliano ya talaka na Uingereza yakiwa pamoja zaidi mara hii, na kwamba kuna msimamo wa pamoja zaidi kuhusiana na muongozo wa majadiliano hayo ambao unapaswa kuidhinishwa katika mkutano wa Jumamosi.
Mara kadhaa yakiwa na misimamo inayotofautiana kuhusiana na masuala muhimu kuanzia wakimbizi hadi katika mzozo wa kifedha, mataifa ya Umoja wa Ulaya yamesema hakuna masuala makubwa ambayo yatawashughulisha viongozi hao katika mkutano huo wa mwishoni mwa juma.
Mwenyekiti wa tume ya majadiliano Michel Banier , amesema kwamba "tuko tayari, tuko tayari" kuingia katika majadiliano , wakati akiingia katika mkutano mjini Luxembourg. Mara muongozo utakapoidhinishwa siku ya Jumamosi, makao makuu ya Umoja wa Ulaya utayaingiza katika muongozo wa majadiliano kwa ajili ya Banier hali ambayo inatakiwa kuwa tayari ifikapo Mei 22.
Wakati wa kuwa pamoja
Mazungumzo yanatarajiwa kuanza baada ya uchaguzi nchini Uingereza utakaofanyika Juni 8.
"Mkutano huo ulikuwa muhimu kwa dhana kwamba ni ishara muhimu ya kuaminiana, umoja na msimamo wa pamoja kwa mataifa hayo 27," amesema naibu waziri mkuu wa Malta Louis Grech , aliyekuwa mwenyekiti wa mkutano wa mawaziri.
"Tumeweka wazi katika muongozo kwamba soko la pamoja halitagawanyika na kwamba hakutakuwa na kuchagua chagua. Nafikiri hilo liko wazi na linaeleweka ndani ya utaratibu wa muongozo. Iwapo wanaota ama kutoota , sitakwenda upande huo. Mimi si mfumbuzi wa siri kujua kama wana mawazo ya kufikirika. Kwa hiyo nafikiri kadri muda unavyokwenda tutafahamu kwa hakika ni msimamo gani kuhusiana na soko la pamoja kuihusu Uingereza."
Wakati bado Umoja wa Ulaya unaiangalia Uingereza kama mshirika wa karibu , kansela wa Ujerumani Angela Merkel alisema mara talaka itakapotolewa na nchi hiyo kujiondoa kutoka Umoja huo nchi hiyo itakuwa nje na kamwe haitakuwa na haki sawa ama kuwa katika nafasi bora kuliko nchi mwanachama wa Umoja huo. " Amesema wanachama wote 27 wa Umoja wa Ulaya na taasisi za Ulaya wanakubaliana kwa hilo."
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape
Mhariri: Yusuf , Saumu