Umoja wa Ulaya waipa Uingereza muda zaidi wa Brexit
22 Machi 2019Baada ya mkutano ambao ulidumu mchana kutwa hadi chakula cha jioni, Umoja wa Ulaya ulisema Uingereza inaweza kuahirisha tarehe ya kujiondoa, ambayo ilikuwa imepangwa Machi 29, hadi Mei 22 – kama bunge la Uingereza litaidhinisha wiki ijayo mpango wa May wa kutalikiana na umoja huo.
Kama mpango huo uliokataliwa mara mbili utatupwa nje tena, Umoja wa Ulaya unasema Uingereza ina hadi Aprili 12 "kuja na pendekezo jingine katika kusonga mbele”. Rais wa Baraza la Ulaya Donald Tusk amesema May ameukubali mpango huo.
Tusk alisema Aprili 12 ndiyo tarehe kamili ya Uingereza kuamua kama inataka kushiriki katika uchaguzi wa mwaka huu wa bunge la Ulaya. Uingereza itahitaji muda wa kuamua bungeni kama itashiriki katika uchaguzi huo wa Mei 23 hadi 26 na Mei amesisitiza kuwa hilo halitawezekana kwa sababu itakuwa kwenda kinyume na uamuzi wa wapiga kura wa kumaliza uwanchama wao wa miaka 46 katika Umoja wa Ulaya
Tusk amesema kama bunge halitaamua basi haitawezekana tena kurefusha mchakato wa Brexit na kuwa hata kukiwa na uchaguzi, mataifa yote yanayobaki 27 wanachama yataidhinisha kwa kauli moja.
Waziri mkuu wa Luxembourg Xavier Bettel alionya kuwa kama Umoja wa Ulaya hautakuwa na jibu kutoka kwa Uingereza ifikapo Aprili 12, basi nchi hiyo itaondoka katika Umoja wa Ulaya bila ya makubaliano.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, ambaye alikuwa amechukua msimamo mkali kuliko baadhi ya viongozi wenzake, alisema jukumu sasa liko mikononi mwa Uingereza.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel aliapa kufanya kazi hadi muda wa mwisho ili kuhakikisha kuwa Uingereza haiondoki bila ya makubaliano, hata ingawa serikali yake imeweka hatua za dharura za kukabiliana na hali kama hiyo.
Wafanyabiashara na wachumi wanasema kama Uingereza itajitoa bila ya makubaliano hali hiyo itasababisha uharibu mkubwa na hasara ya mabilioni kwa uchumi wa Uingereza na Umoja wa Ulaya. Chama cha Viwanda nchini Uingereza na Chama kikuu cha Wafanyakazi vimesema katika taarifa ya pamoja kuwa nchi hiyo inakabiliwa na janga la kitaifa.
Hata wakati akikutana na viongozi wa mataifa 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya mjni Brussels kwa mkutano wa kilele wa Baraza la Ulaya, waraka wa mtandaoni uliosimamiwa na bunge la Uingereza ukitaka mchakato wa Brext usitishwe ulipata Zaidi ya saini milioni mbili. Bado haijafahamika wazi kama mpango wa kujiondoa wa May aliosaini na Umoja wa Ulaya Novemba mwaka jana utapitishwa bungeni.
Mpango wa May bado unakabiliwa na upinzani miongoni mwa wabunge wa pande zote za mdahalo wa Brext, huku baadhi wakihoji kuwa unaiweka Uingereza karibu sana na Umoja wa Ulaya, na wengine wakisema hautaiweka karibu sana. Wapiga kura wa Uingerezapia wanatofautiana vikali. Wengi wa wanaoegemea Umoja wa Ulaya wanaunga mkono hatua ya kucheleweshwa Brexit kwa muda mrefu, wakiamini kuwa itaongeza shinikizo nyumbani ili kufanyika uchaguzi mkuu au kura ya pili ya maoni ambayo huenda ikaubatilisha uamuzi wa kujiondoa Ulaya.