Umoja wa Ulaya waitaka Syria kusitisha mashambulizi Idlib
21 Februari 2020Baraza la Umoja wa Ulaya limesema Ijumaa kuwa mashambulizi ya kijeshi katika jimbo la Idlib yanayofanywa na serikali ya Syria pamoja na washirika wake yanasababisha mateso makubwa kwa binaadamu na kwamba mashambulizi hayo hayakubaliki.
Wakati mvutano ukiongezeka kati ya Urusi na Uturuki, Umoja wa Ulaya umetoa wito wa kusitishwa mara moja mapigano kati ya pande zote zinazohasimiana na kuheshimu sheria ya kimataifa ya haki za binaadamu ili kuruhusu huduma za kibinaadamu kuwafikia raia wanaohitaji msaada.
Yanayoendelea Idlib hayapaswi kupuuzwa
Tahadhari hiyo imetolewa wakati wa mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya ambao unalenga kuijadili bajeti ya umoja huo. Wakati akiwasili kwenye mkutano huo, Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron amesema matukio yanayoendelea kaskazini magharibi mwa Syria ambako vikosi vya serikali ya Rais Bashar al-Assad vinataka kushinda katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka tisa, hayawezi kupuuzwa.
''Hatuwezi kukutana leo kana kwamba hakuna chochote kilichotokea kilomita chache kutoka hapa. Leo na kwa wiki kadhaa mzozo mbaya kabisa wa kibinaadamu umekuwa ukiendelea nchini Syria. Nalaani vikali mashambulizi ya kijeshi yanayofanywa na utawala wa al-Assad dhidi ya raia wa Idlib,'' alifafanua Macron.
Macron amelitolea wito Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo Ufaransa ni mwanachama wa kudumu kulishughulikia suala hilo, baada ya Urusi kuzuia kulipitisha pendekezo linalotaka kusitishwa kwa mapigano. Mashambulizi yanayofanywa na vikosi vya Rais Assad yanakusudia kuyachukua tena maeneo ya mwisho yanayodhibitiwa na waasi.
Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel na Rais Macron Alhamisi walizungumza na Rais wa Urusi, Vladmir Putin na kupendekeza yafanyike mazungumzo ya haraka na Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan ili kupunguza mvutano uliopo. Aidha, Umoja wa Ulaya umesema uko tayari kuongeza msaada kwa raia walio hatarini zaidi ambao wameathirika na mashambulizi hayo.
Watu 900,900 hawana makaazi
Umoja wa Mataifa umesema mashambulizi hayo yamesababisha watu 900,000 kuyakimbia makaazi yao, tangu Desemba Mosi, huku zaidi ya 500,000 kati ya hao wakiwa ni watoto. Wafanyakazi wa mashirika ya misaada wametoa wito wa kusitishwa mapigano na wameomba msaada wa kimataifa kuwasaidia karibu watu milioni moja wanaoyakimbia makaazi yao.
Wakati huo huo, wizara ya ulinzi ya Uturuki imesema wanajeshi wake wawili wameuawa katika shambulizi la anga kwenye jimbo la Idlib. Wizara hiyo imesema wanajeshi watano wamejeruhiwa katika shambulizi hilo lililokuwa likiyalenga majeshi ya Uturuki. Mauaji hayo yanaifanya idadi jumla ya wanajeshi wa Uturuki waliouawa hadi sasa kufikia 15.
(AFP, AP, DPA)