Umoja wa Ulaya waitaka Uturuki kuheshimu haki za binadamu
26 Julai 2017Baada ya mkutano uliofanyika mjini Brussels, Kamishina wa Umoja wa Ulaya anayehusika na utanuzi wa nchi wanachama ndani ya Umoja huo Johannes Hahn alionesha wasiwasi wake juu ya hatua ya kuwekwa kizuizini watu hao wakati Waziri wa Mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu alitetea uamuzi huo akisema ni hatua ya lazima katika mapambano dhidi ya makundi ya itikadi kali.
Uturuki imekuwa katika mgogoro wa kidiplomasia na Umoja wa Ulaya pamoja na mshirika mwenzake katika NATO Ujerumani, kufuatia hatua ya nchi hiyo kuwatia mbaroni wiki iliyopita wanaharakati wa haki za binadamu akiwemo raia mmoja wa Ujerumani wakihusishwa na makosa ya ugaidi.
Awali mjerumani mwenye asili ya Uturuki alikamatwa akidaiwa kufanya upelelezi na kuwasaidia waasi wa kikurdi. Kabla ya mazungumzo hayo kuanza mjini Brussels, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alisema kuwa zama za Uturuki kukubali shinikizo kutoka mataifa ya nchi za magharibi sasa zimefikia kikomo.
Mkutano huo wa Brussels ulijikita zaidi katika masuala kadhaa yakiwemo ombi la muda mrefu la Uturuki kutaka kuwa mwananchama wa Umoja wa Ulaya, mapambano dhidi ya ugaidi, nishati pamoja na mahusiano ya kibiashara ingawa pia umeitishwa mnamo wakati serikali ya Uturuki ikiendelea na operesheni dhidi ya watu inaowatuhumu kuhusika na jaribio la mapinduzi lililoshindwa la mwaka jana.
Zaidi ya watu 50,000 wakiwemo waandishi wa habari na wanasiasa wa upinzani wametiwa mbaroni tangu wakati wa jaribio hilo la mapinduzi lililoshindwa Julai 15, 2016.
Wakosoaji wanasema operesheni hiyo awali iliwalenga viongozi wanaohusishwa na jaribio la mapinduzi lakini sasa imetanuka zaidi ikiwalenga pia wapinzani wa serikali.
Uturuki yatakiwa kuheshimu haki za binadamu
Umoja wa Ulaya unataka kuhakikisha Uturuki inaheshimu haki za binadamu, utawala wa sheria, demokrasia na haki za msingi ikiwa ni pamoja na uhuru wa vyombo vya habari.
Aidha Umoja wa Ulaya umeonesha wasiwasi wake kuhusiana na hatua ya serikali ya Uturuki kuwakamata na kuwatia gerezani waandishi habari kadhaa, wahadhiri, wanasheria na watetezi wa haki za bindamu.
Hata hivyo waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu alitetea kukamatwa kwa wanaharakati pamoja na waandishi wa habari akisema walikamatwa kutokana na kushukiwa kuhusika na makundi ya itikadi kali.
Uturuki iliomba kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya miongo mitatu iliyopita na kuanza majadiliano kuhusiana na suala hilo mwaka 2005.
Kwa upande wake waziri wa Uturuki anayehusika na masuala ya Umoja wa Ulaya Omer Celik amesema majadiliano hayo ya Jumanne wiki hii yalikuwa ya mafanikio ingawa alikiri kuwa kuna maeneo ambayo hawakukubalina na kuongeza kuwa bado wataendelea kujadiliana.
Mwandishi: Isaac Gamba/ape/eap
Mhariri: Bruce Amani