Umoja wa Ulaya waiwekea vikwazo Sudan Kusini
11 Julai 2014Taarifa ya Umoja wa Ulaya iliyotolewa mapema Ijumaa, imetangaza kumuwekea vikwazo Peter Gadet ambaye ni kiongozi wa jeshi la waasi kutoka kabila la Nuer, ambaye pamoja na mengine inamtaja kuwa kikwazo cha kupatikana amani ya kudumu katika nchi hiyo ambayo imekuwa ikikabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe tokea ipate uhuru wake miaka mitatu iliyopita.
Inasemekana Gadet, aliyewekewa vikwazo pia na Marekani mwezi Mei mwaka huu, alipanga na kuongoza mashambulizi katika mji wa Bentiu ambayo yalisababisha watu wapatao 200 kuuwawa.
"Peter Gadet anahusika katika kuchochea machafuko, kuzuia mchakato wa kisiasa Sudan Kusini pamoja na matukio ya ukiukaji wa haki za binadamu," ilisema ripoti hiyo ya Umoja wa Ulaya.
Vikwazo vya matumizi ya silaha
Kwa upande wa jeshi la serikali, taarifa hiyo ya Umoja huo imesema imemuwekea vikwazo Santino Deng ambaye alikiuka makubaliano ya kusitisha vita yaliyosainiwa Januari 23 mwaka huu.
Katika taarifa yake nyingine iliyotoka mapema Ijumaa, Umoja wa Ulaya umesema kikwazo juu ya matumizi ya silaha kipo pale pale licha ya kwamba Umoja huo umebaini kuwa jeshi la serikali na waasi wameendelea kupokea silaha ambazo wamekuwa wakizitumia katika mapigano kati yao.
Umoja huo wa Ulaya umesema endapo pande hizo mbili zinazohasimiana hazitoheshimu mkataba wa kusitisha mapigano uliotiwa saini tarehe 23 Januari na kurudiwa tena tarehe 9 Mei, itatoa vikwazo zaidi kwa kila upande.
Zaidi ya watu millioni 1.5 hawajulikani walipo huku takribani watu 10,000 wameuwawa tokea kuanza kwa mapigano ya kugombania madaraka kati ya jeshi la serikali ya Sudan Kusini inayoongozwa na Salva Kiir dhidi ya waasi wanaoongozwa na aliyekuwa makamu wa rais wa nchi hiyo Riek Machar.