Umoja wa Ulaya wakosoa ukandamizaji wa upinzani Uganda
21 Januari 2021Umoja wa Ulaya umeelezea masikitiko juu ya unyanyasaji na ukandamizwaji uliofanyiwa wanasiasa wa upinzani, wafuasi wao, watendaji wa mashirika ya kiraia pamoja na vyombo vya habari.
Taarifa ya umoja huo imeitaka serikali ya Uganda kutimiza wajibu wake wa kimataifa kwa kuhakikisha kwamba vikosi vya usalama vinajizuia kutumia nguvu kupita kiasi na kuchunguza vitendo vyote vya ukiukaji wa haki za watu
Kadhalika Umoja wa Ulaya umetoa wito kwa serikali mjini Kampala kuheshimu uhuru wa watu kujieleza na haki ya kuandamana na kukusanyika kwa amani, ikiwemo uhuru wa kutembea kwa wanasiasa na wafuasi wao.
Hayo yanajiri wakati aliyekuwa mpinzani mkuu wa rais Yoweri Museveni katika uchaguzi wa wiki iliyopita Robert Kyagulanyi akisalia kizuizini tangu alipopiga kura licha ya miito ya kutaka kuachiwa kwake.
Kwenye uchaguzi huo Museveni alitangazwa mshindi lakini upinzani umeyapinga matokeo hayo ukisema uchaguzi ulikumbwa na vitendo vya udanganyifu.