Umoja wa Ulaya walaumiwa kwa kukwamisha biashara kati ya nchi maskini
16 Septemba 2007Halmashauri ya Umoja wa Ulaya ina matumaini ya kusaini mikataba kadhaa ya kibiashara ya EPA na nchi 76 za Afrika, Karibik na Pacific, ACP, kufikia mwishoni mwa mwaka huu. Huku nchi za Karibik zikiwa zimeashiria kuwa tayari kukubali tarehe ya mwisho iliyowekwa yaani Disemba 31, mpatanishi wake na Umoja wa Ulaya, mjumbe wa Jamaica, Junior Lodge, anasema kuna mambo muhimu yanayohitaji kutatuliwa.
Kwa mujibu wa mapendekezo ya mikataba ya kibiashara ya EPA, halmashauri ya Umoja wa Ulaya inataka kila mikataba ya kibiashara ambayo nchi za Karibik itasaini na nchi yoyote duniani inayouza zaidi ya asilimia moja ya bidhaa zinazouzwa katika soko la kimataifa, kama vile China, Uturuki, India na Brazil, sharti mikataba hiyo isainiwe kwa kushaurina na halmashauri hiyo.
Junior Lodge amesema sharti hili huenda lilizuie eneo la Karibik kuifanya kuwa huru biashara yake ya pombe kali na India na Brazil bila kuweka kanuni sawa kwa Ulaya ambayo pia huuza pombe kali. Mjumbe huyo wa Jamaica anadai msimamo wa Umoja wa Ulaya kuhusu swala hili unasababishwa na kile kiitwacho sera ya kimataifa ya Ulaya.
Sera hiyo iliyozinduliwa mwaka jana, inautaka Umoja wa Ulaya uonde vikwazo vyote vinavyozikabili kampuni za nchi za magharibi zinazotaka kufanya biashara katika nchi za kigeni, ikiwa ni pamoja na vikwazo vinavyonuiwa kuzilinda kampuni za ndani katika nchi maskini. Lodge amesema wanaipinga vikali sera hiyo.
Wajumbe wa eneo la Karibik pia wanakabiliwa na sharti lingine la Umoja wa Ulaya linalotaka nchi za Karibik zisitumie vipindi vya kutotoza kodi kuwavutia wawekezaji wa kigeni. Lodge amependekeza kwamba Umoja wa Ulaya una upendeleo kwa kuwa nchi mbili wanachama wa umoja huo, Jamhuri ya Cheki na Estonia, zimetumia sana njia hiyo ya kuvutia wawekezaji.
Pia mjumbe huyo ameeleza wasiwasi wake juu ya ombi la Umoja wa Ulaya kutaka orodha ya raia wa umoja huo walio na akaunti za benki katika nchi za Karibik. Amesema Bahamas ina hofu Umoja wa Ulaya unajaribu kufungua sekta ya huduma za fedha.
Hali ya sasa ya mikataba ya EPA ilijadiliwa na wajumbe wa Umoja wa Ulaya na nchi za ACP kwenye mkutano uliofanyika tarehe 12 na 13 mwezi huu mjini Brussels, Ubelgiji. Hans Joachim Keil, waziri wa biashara wa Samoa na kiongozi wa ujumbe wa nchi za Pacific, alisema sheria kuhusu bidhaa zinakotoka zinazotekelezwa na Umoja wa Ulaya kuhusu uuzaji wa bidhaa katika nchi za Pacific zinahitaji kufanyiwa marekebisho.
Kwa sasa bidhaa kutoka nchi za ACP kimsingi zinaruhusiwa kuingia soko la Umoja wa Ulaya bila kutozwa kodi lakini hilo limebakia katika makaratasi kwani halifanyiki. Bidhaa kutoka nchi za ACP zinazotumia malighafi kutoka sehemu nyingine za dunia haziruhusiwi kuingia soko la Ulaya kama bidhaa za nchi iliyozitengeneza bidhaa hizo.
Kwa mfano shati inayotengenezwa nchini Fiji kutumia pamba kutoka India inaorodheshwa kuwa bidhaa ya India kwa mujibu wa sheria za Umoja wa Ulaya. Swala hili limeelezwa kuwa tete na ikiwa halitatuliwa huenda kusipatikane makubaliano.
Boyce Sebetela, mbunge wa Botwana amesema inazidi kudhihirika wazi kwamba mikataba ya EPA inahitaji kufanyiwa marekebisho. Aidha mbunge huyo amesema masharti ya Umoja wa Ulaya ndiyo yanayotawala huku matakwa ya nchi za Afrika, Karibik na Pacific yakipuuzwa. Ingawa nchi za ACP ziko huru na zimejikomboa kisiasa ipo haja ya kuanzisha mapinduzi ya kiuchumi ili wananchi katika nchi hizo wanufaike kutokana na mikataba ya EPA.