1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Umoja wa Ulaya watafakari uanachama wa Ukraine

6 Novemba 2023

Maafisa wa Umoja wa Ulaya wamesema wanatarajia kupendekeza kuipeleka Ukraine kwenye hatua moja karibu na kuwa mwanachama wa umoja huo wiki hii.

https://p.dw.com/p/4YRyd
Ursula von der Leyen na Volodymyr Zelenskiy
Rais wa EU Ursula von der Leyen (kushoto) na Rais Volodymyr Zelenskiy (kulia)Picha: Efrem Lukatsky/AP Photo/picture alliance

Haya yanafanyika wakati ambapo Urusi imeishambulia Ukraine kwa makombora na ndege zisizokuwa na rubani usiku wa kuamkia Jumatatu na kusababisha majeraha ya watu kadhaa.

Mnamo Jumatano wiki hii, afisi ya Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen itachapisha ripoti inayoangazia hatua ilizopiga Ukraine katika azma yake ya kutaka kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya.

Mkutano wa kilele wa EU Desemba

Akizungumza baada ya kukutana na Rais wa UkraineVolodymyr Zelenskiy mwishoni mwa wiki mjini Kyiv, Von der Leyen alisema.

"Nataka nikwambie jinsi tulivyoridhika na mageuzi muliyoyafanya wakati munapopigana vita musivyostahili kuvisahau. Munapigana na wakati huo huo munaibadilisha pakubwa nchi yenu. Mumepiga hatua kubwa kuubadilisha mfumo wenu wa haki, kuikomboa nchi yenu kutoka kwenye mikono ya mabwenyenye na kukabiliana na utakatishaji wa fedha," alisema Von der Leyen.

Ukraine Kyiv | Ziara ya von der Leyen |  Hotuba yake bungeni
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der LeyenPicha: Andrii Nesterenko/REUTERS

Ripoti hiyo itakayotolewa itakuwa muhimu kwa maamuzi yatakayofanywa na viongozi wa mataifa ya Umoja wa Ulaya katika mkutano wa kilele utakaofanyika Desemba, kuamua iwapo kuanze mazungumzo rasmi ya kuijumuisha Ukraine katika umoja huo. Ripoti hiyo pia itaziangazia nchi za Georgia na Moldova.

Mazungumzo hayo kwa kawaida huchukua miaka kabla nchi zinazoomba uanachama kuvitimiza vigezo vya kisheria na kiuchumi vya kujiunga, na Umoja wa Ulaya haupo tayari kuijumuisha kama mwanachama wake nchi ambayo iko vitani.

Wakati huo huo, maafisa wa Ukraine katika Bahari Nyeusi wamesema mashambulizi ya Urusi ya ndege zisizokuwa na rubani usiku wa kuamkia Jumatatu, yamesababisha majereha ya watu watano, yakateketeza malori yenye nafaka na kuharibu mojawapo ya makumbusho ya sanaa katika mji huo.

Urusi kufanya mashambulizi msimu wa baridi

Kuna hofu inayoongezeka nchini Ukraine kwa sasa kwamba Urusiitashambulia miundo mbinu ya nishati kama ilivyofanya kipindi kilichopita cha majira ya baridi, ambapo mifumo ya kuleta joto majumbani na huduma za umeme vilitatizwa kwa mamilioni ya watu.

Vita vya Ukraine I Shambulizi la Urusi mjini Kyiv
Uharibifu uliofanywa na kombora la Urusi mjini KyivPicha: Valentyn Ogirenko/REUTERS

Ukraine imekuwa ikitoa wito kwa marafiki zake wa nchi za Magharibi kuipa misaada zaidi hasa ya mifumo ya kujilinda angani, kuelekea mashambulizi zaidi yanayotarajiwa ya Urusi katika msimu wa baridi.

Hayo yakiarifiwa Ukraine imesema imeanzisha uchunguzi baada ya kombora la Urusi kusababisha vifo vya wanajeshi kadhaa katika kile ambacho ripoti za vyombo vya habari zinasema ilikuwa ni hafla ya kuwatuza wanajeshi hao.

Karibu wanajeshi 20 wanaripotiwa kuuwawa katika shambulizi hilo ambalo vyombo vya habari vya Ukraine vinasema lilifanyika Ijumaa iliyopita.

Vyanzo: Reuters/AFP