1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Afrika kuathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabia nchi

2 Machi 2022

Japo Afrika inachangia kiasi kidogo utoaji gesi chafuzi, bara hilo limeathiriwa pakubwa na athari za mabadiliko ya tabia nchi, ikiwa ni pamoja na ukame, mafuriko na njaa.

https://p.dw.com/p/47sOQ
Flash-Galerie Schatten
Picha: picture-alliance/maxppp/wostock press

Kulingana na ripoti iliyotolewa wiki hii na Umoja wa Mataifa, hali itaendelea kuwa mbaya kwa bara hilo katika miaka ijayo. 

Mnamo Jumatatu, jopo la Umoja wa Mataifa linalozileta pamoja serikali mbalimbali kuhusu mabadiliko ya tabia nchi-IPCC, lilitahadharisha kwamba mafuriko, joto kali na kiangazi ni majanga ambayo yataongezeka kusini mwa jangwa la Sahara.

Ripoti ya IPCC: Dunia yashindwa kudhibiti uzalishaji gesi chafu

Kwamba wanyama pori na mimea vilevile itapungua. Utabiri huo ulieleza zaidi kwamba theluji katika vilele vya milima mathalan Ruwenzori na Kilimanjari zitatoweka katika miongo ijayo.

Ikizingatiwa bara la Afrika tayari linazongwa na viwango vya juu vya umaskini, ukosefu wa chakula cha kutosha, jopo hilo limetahadharisha kwamba wavuvi na wakulima wataathiriwa, na mavuno hayataweza kuyakidhi mahitaji yao.

COP26: Makubaliano yalegeza msimamo kuhusu makaa ya mawe

Nchini Kenya, Safari Mbuvi ambaye ni mkulima anakabiliwa na changamoto zinazotokana na ukame ambao umeshadumu kwa miaka minne. Mara kwa mara mimea yake shambani haijakuwa ikifanya vyema.

Wanyama pori ni miongoni mwa viumbe vinavyotarajiwa kuathiriwa pakubwa kufuatia athari zaa mabadiliko ya tabia nchi.
Wanyama pori ni miongoni mwa viumbe vinavyotarajiwa kuathiriwa pakubwa kufuatia athari zaa mabadiliko ya tabia nchi.Picha: DW

”Tangu nilipokuwa mdogo, baba yangu alikuwa akipata mavuno mengi katika shamba hili. Lakini sasa, yaonekana kuna mabadiliko ya tabia nchi. Mvua ni chache na hazitabiriki. Sitapata mavuno mazuri wakati huu hata gunia moja la mahindi sitaweza kupata. Si mimi pekee yangu ninayekumbwa na hali kama hii bali  kila mkulima. Kila mkulima katika Eneo hilo amepata hasara kubwa.” Amesema Mbuvi.

IPCC: Gharika zinatokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi

Ripoti ya Umoja wa Mataifa imeeleza kwamba ongezeko la joto litadhuru mfumo wa uzalishaji chakula barani Afrika na litasababisha uhaba wa maji na vipindi vya upanzi vitakuwa vifupi. Mazao kama mtama, kahawa, chai na hata idadi ya mifugo yatapungua.

Jopo hilo liliongeza kuwa tangu mwaka 1961, mazao kutokana na kilimo yamepungua kwa asilimia 34 kufuatia athari za mabadiliko ya tabia nchi. Hiyo ikiwa athari ya juu zaidi kuliko hali katika kanda nyinginezo.

Tangu mwaka 2012 idadi ya watu ambao wamekumbwa na ukosefu wa lishe bora kusini mwa jangwa la Sahara imeongezeka kwa asilimia 45.6%, kulingana na shirika la mpango wa Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa.

Je mabadiliko ya tabia nchi yamechangia mafuriko?

Pamoja na mabadiliko ya tabia nchi, migogoro, machafuko na misukosuko ya kiuchumi pia imechangia njaa.
Pamoja na mabadiliko ya tabia nchi, migogoro, machafuko na misukosuko ya kiuchumi pia imechangia njaa.Picha: DW

Mnamo mwaka 2020, watu milioni 98 barani Afrika walikumbwa na uhaba mkali wa chakula na walihitaji misaada ya kiutu. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya ulimwengu kuhusu migogoro kutokana na uhaba wa chakula na vilevile kulingana na Mpango wa Chakula Duniani (WFP).

Jopo la IPCC limeonya kwamba ikiwa viwango vya joto ulimwenguni vitaongezeka kwa Celsius 1.8 ifikapo mwaka 2050, basi watoto milioni 1.4 zaidi wa Afrika watadumaa kufuatia ukosefu wa lishe bora.

Ukosefu wa chakula kusini mwa jangwa la Sahara na hali ya utapiamlo unahusishwa zaidi na viwango vya juu vya joto na ukosefu wa mvua ya kutosha katika kanda za Afrika magharibi na kati.

Dunia inahitaji hatua thabiti za kulinda mazingira

Wanasayansi wanasema ni vigumu zaidi kujaribu kutenganisha umaskini unaoikumba Afrika na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Jean Paul Adam anayeongoza idara ya mabadiliko ya tabia nchi katika Umoja wa Mataifa kwa Afrika, amesema Afrika ina asilimia 17 ya idadi jumla ya watu ulimwenguni- na inatoa tu asilimia 4 ya gesi chafu. Licha ya hayo ndilo bara ambalo limeshaathiriwa mno na mabadiliko ya tabia nchi. Ukosefu wa mikakati imara ya kudhibiti athari hizo pia imetajwa kuchangia hali hiyo.

(AP)