UN: Dunia inapaswa kujiandaa kwa joto linaloongezeka
18 Julai 2023Umoja wa Mataifa umeonya hii leo kuwa dunia inapaswa kujiandaa kwa mawimbi yanayoongezeka ya joto, huku mataifa ya ncha ya Kaskazini yakikabiliana na joto la kupindukia. Mshauri mwandamizi wa shirika la hali ya hewa la Umoja wa Mataifa, WMO, John Nairn, amewaambia waandishi kuwa matukio haya yataendelea kukua katika uzito, na kwamba dunia inapaswa kujiandaa kwa mawimbi makali zaidi.
Watoto 1,200 wahamishwa Ugiriki kutokana na joto kali
Matamshi yake yamekuja wakati Ulaya ikijiandaa kwa joto kali zaidi leo, chini ya mawimbi ya joto na mioto ya nyika ambavyo vimeyakumba maeneo makubwa ya ncha ya kaskazini, na kulaazimu kuhamishwa kwa watoto 1,200 karibu na kisiwa cha Ugiriki.
Watu wahimizwa kunywa maji
Mamlaka za afya zimetoa tahadhari kuanzia Amerika Kaskazini hadi Ulaya na Asia, zikiwahimiza watu kunywa maji kwa wingi na kujiepusha na jua kali, katika ukumbusho mzito juu ya madhara ya joto dunia.