UN: Hali nchini Ethiopia inazidi kuwa mbaya
10 Desemba 2020Tamko la mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet amelitowa jana ambapo ameielezea hali ya Tigray kuwa ya wasiwasi mkubwa sana na ni tete kutokana na vita ambavyo vinaendelea kuripotiwa katika maeneo yanayouzunguka mji mkuu wa jimbo hilo Mekele, na miji ya Sheraro na Axum, licha ya serikali kudai kinyume chake.
Mkuu huyo wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa anasema wana taarifa za uhakika kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu na unyanyasaji ikiwemo mashambulizi ya kiholela dhidi ya raia na majengo ya kiraia, uporaji, utekaji nyara na unyanyasaji wa kingono dhidi ya wanawake na wasichana.
Soma zaidi: Umoja wa Ulaya waitaka Ethiopia irudishe mawasiliano Tigray
Bachelet ameonya kwamba ni hali inayoshindwa kudhibitiwa na kunahitajika uangalizi wa dharura kutoka nje. Hata hivyo, Ethiopia imeshaikataa miito hiyo ya kupelekwa wachunguzi huru katika mapigano yaliyosababisha mauaji katika jimbo hilo la Tigray.
Ethiopia inasema haihitaji mlezi kama mtoto mdogo. Miito inaongezeka ya kutaka uwepo uwazi zaidi katika vita hivyo kati ya wanajeshi wa serikali kuu ya Ethiopia na wale wa serikali ya jimbo la Tigray ambayo inadhaniwa kwamba imewauwa maelfu ya watu wakiwemo raia.
Ethiopia imekata miito ya kupelekwa wachunguzi huru
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rigths Watch alau limefanikiwa kuorodhesha matukio ya mojawapo ya mauaji makubwa na inahofiwa kwamba kuna matukio mengine zaidi kama hayo.
Hata hivyo afisa mmoja mwandamizi wa serikali ya Ethiopia Redwan Hussein aliwaambia waandishi habari siku ya Jumanne jioni kwamba nchi hiyo itakaribisha msaada pale tu itakapohisi imeshindwa kufanya uchunguzi, lakini kufikiria tu kwamba haiwezi kumudu kufanya uchunguzi ni kuidharau serikali''.
Ingawa sio wito tu wa kufanyika uangalizi wa dharura Ethiopia unaotolewa na Umoja wa Mataifa, kwa wiki kadhaa sasa umoja huo unazungumzia suala la kuruhusiwa mashirika ya kutowa msaada kuingia Tigray. Katibu Mkuu wa umoja huo, Antonio Guterres amesema tathmini ya pamoja na serikali ya Ethiopia itafanyika ili kuhakikisha mashirika hayo yanaweza kuyafikia maeneo yote ya Tigray kuanza shughuli ya kutowa msaada.
Kadhalika katibu mkuu Guterres amesema hali nyingine ya ghadhabu inaongezeka wakati jimbo hilo la Tigray likiendekea kwa kiasi kikubwa kutenganishwa na ulimwengu,huku watu milioni 6 wakihitaji chakula,na dawa na wengine kiasi milioni 1 wakitajwa kuachwa bila makaazi.
Njia za mawasiliano zimekatwa na barabara za kutoka na kuingia jimbo hilo bado zikiwa zimefungwa hali ambayo inazuia kuonekana ni kwa kiasi gani yalivyo mauaji yaliyosababishwa na operesheni ya kijeshi ya waziri mkuu Abiy Ahmed dhidi ya TPLF iliyoanza tarehe 4 Novemba.