UN kuiwekea vikwazo Sudan Kusini
13 Julai 2018Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litapiga kura leo Ijumaa, juu ya azimio ambalo linaweka vikwazo vya silaha kwa Sudan Kusini, na vikwazo dhidi ya mkuu wa sasa wa ulinzi na mkuu wa zamani wa jeshi. Rasimu ya azimio la mwisho iliyopatikana siku ya Alhamis inaelezea wasiwasi mkubwa wa viongozi wa Sudan Kusini kushindwa kumaliza vita, ukiukwaji wa haki za binadamu unaoendelea nchini humo unaotishia kutomalizika kwa mapigano.
Azimio hilo lililowasilishwa na Marekani linahitaji kura chache za ndio zinazohitaji kupitishwa na baraza la wanachama 15, huku wanadiplomasia wakisema wanatarajia kutokuwepo kwa baadhi ya wajumbe ingawa hakutakuwa na kura ya turufu.
Kulikuwa na matumaini makubwa kwamba Sudan Kusini itakuwa na amani na utulivu baada ya uhuru wake kutoka taifa jirani la Sudan mwaka 2011, lakini taifa hilo jipya kabisa duniani liliingia katika migogoro pamoja na unyanyasaji wa wakimbizi mwezi Disemba mwaka 2013, wakati majeshi yanayomtii Rais Salva Kiir yalipoanza kuwashambulia wale wanaomtii Riek Machar ambaye alikuwa makamu wake.
Mpango wa amani uliosainiwa Agosti 2015, haukumaliza vita wala uadui. Rasimu hiyo la azimio la mwisho pia ilieleza kuwa, usafirishaji wa silaha ni hatari kwani unachochea migogoro na mapigano nahivyo kuhimiza nchi zote mbili kuchukua hatua ya haraka kutambua na kuzuia uingizwaji wa mizigio katika mipaka yao.
Wakati huo huo, Shirika la Haki za Binaadamu la Human Rights Watch limelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutokuyapuuzia matukio ya kihalifu yanayoendelea kutokea Sudan Kusini. Katika ripoti yake iliyotolewa leo, shirika hilo linasema kuwa kuna mateso makubwa yanayowakumba raia wa Sudan Kusini kutoka kwa seriklai yao.
Ripoti za kamishina mkuu wa haki za binadamu na ile ya ujumbe wa amani wa umoja wa mataifa Sudan Kusini UNMISS zimeorodhesha visa vya kutekwa, kubakwa na matukio mengine ya kikatili yanayofanywa na wanajeshi wa Sudan Kusini wakati wa operesheni ya kijeshi iliyofanyika kati ya mwezi Aprili na Mei.
Human Rights Watch wanasema kwenye taarifa yake ya leo, kwamba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lina fursa nzuri ya kugeuza maonyo yake kuwa katika vitendo.
Mwandishi: Veronica Natalis/ AFP/HRW
Mhariri: Mohammed Khelef