UN kupigia kura azimio la kuwapeleka wachunguzi Aleppo
18 Desemba 2016Wawakilishi wa waasi wameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP makubaliano yalifikiwa kuruhusu watu wengi zaidi kuondoka katika eneo hilo ambalo limeharibiwa kutokana na mapigano mabaya kabisa kutokea katika vita vya miaka sita sasa ambavyo vimewauwa zaidi ya watu 310,000. Lakini hakuna uthibitisho kutoka utawala wa rais Bashar al-Assad ama washirika wake wakubwa Urusi na Iran, ambao wako katika mbinyo mkubwa wa kimataifa kufikisha mwisho kile rais Barack Obama anachoshutumu kuwa ni "hali ya kuogofya" mjini Aleppo.
Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa linatarajiwa kuketi mchana leo Jumapili kupigia kura pendekezo la Ufaransa la kuwapeleka waangalizi wataoasimamia zoezi la kuwaondoa watu na wataripoti kuhusu ulinzi wa raia, lakini pendekezo hilo linakabiliwa na upinzani kutoka kwa Urusi ambayo ina kura ya turufu.
Balozi wa Ufaransa Francois Delattre amesema kuwapo kwa kikosi cha jumuiya ya kimataifa kutazuwia Aleppo kugeuka kuwa Srebrenica, ambako maelfu ya Wabosnia wanaume na vijana waliuwawa mwaka 1995 wakati mji huo ulipokamatwa na majeshi ya Waserbia wa Bosnia wakati wa vita vya Balkan .
"Lengo letu kwa mswada huu wa azimio ni kugeuka kitu kingine kama Srebrenica katika awamu hii haraka kufuatia operesheni za kijeshi," Delattre ameliambia shirika la habari la AFP. Familia zililala nje usiku kucha katika baridi kali katika majengo ambayo yameharibiwa kwa mabomu katika wilaya ya Al-Amiriyah mjini Aleppo, eneo ambalo ndio linatumika kuwaondoa watu kabla ya zoezi hilo kusitishwa siku ya Ijumaa, ameripoti mwandishi wa habari wa AFP. Abu Omar amesema baada ya kusubiri nje katika baridi kali kwa masaa tisa siku iliyopita, amerejea Jumamosi na kuambiwa kwamba mabasi hayatakuja kuwaondoa.
Hali ya chakula ni mbaya
"Hakuna chakula tena ama maji ya kunywa, na hali inaendelea kuwa mbaya kila siku," amesema, na kuongeza kwamba watoto wake wanne ni wagonjwa kutokana na baridi.
Dazeni kadhaa za malori yakiwa na msaada wa kiutu yalivuka mpaka wa Uturuki siku ya Jumamosi kuingia Syria , na kuweka misaada hiyo katika maeneo salama yaliyotengwa.
Serikali inawalaumu waasi kwa kusitishwa kwa zoezi hilo la kuondolewa ambalo lilianza siku ya Alhamis, ikisema walijaribu kupitishwa kwa magendo silaha nzito na mateka. Upinzani unaishutumu serikali kwa kusitisha zoezi hilo kujaribu kupata kuondolewa kwa wakaazi kutoka Fuaa na Kafraya, vijiji viwili vilivyoko chini ya mzingiro wa waasi katika miji ya Madaya na Zabadani katika jimbo la Damascus ambayo imezingirwa na majeshi ya serikali.
Al-Farook Abu Bakr, kutoka kundi lenye msimamo mkali la waasi la Ahrar al-Sham, amesema makubaliano yalifikiwa kwa ajili ya kuanza tena kuwaondoa raia.
"Kutakuwa na uondoaji wa watu kutoka Fuaa na Kafraya , pamoja na Madaya na Zabadani , na wakaazi wote wa Aleppo na wapiganaji wataondoka," amesema. Lakini serikali haijatangaza makubaliano yoyote. Mjumbe wa Umoja wa Mataifa Staffan de Mistura anakadiria kwamba kuanzia Alhamis raia 40,000 na huenda zaidi ya wapiganaji wapatao 5,000 bado wanaendelea kuwapo katika eneo la Aleppo mashariki. Afisa wa Uturuki amesema watu 90 waliojeruhiwa kutoka Aleppo waliingia Uturuki kwa ajili ya matibabu tangu siku ya Alhamis.
Mwandishi: Sekione Kitojo / AFP
Mhariri: Bruce Amani