UN kupigia kura mswada kuhusu Jerusalem
17 Desemba 2017Misri imesambaza mswada huo Jumamosi (16.12.2017), na wanadiplomasia wamesema baraza huenda likapiga kura kuhusiana na mapendekezo hayo mapema hata Jumatatu.
Akijitoa katika mwelekeo wa kimataifa , rais wa Marekani Donald Trump mwezi huu alitangaza kwamba atautambua mji wa Jerusalem katika mji mkuu wa Israel na kuhamishia ubalozi wa Marekani katika mji huo kutoka Tel Aviv, hatua hiyo imezusha maandamano na shutuma kali.
Mswada huo wa azimio uliopatikana na shirika la habari la AFP unasisitiza kwamba Jerusalem ni suala , "ambalo linaamuliwa kupitia majadiliano" na kueleza "masikitiko makubwa katika uamuzi wa hivi karibuni kuhusiana na hadhi ya mji wa Jerusalem," bila kutaja moja kwa moja uamuzi wa rais Trump.
"Uamuzi wowote na hatua ambazo zitaonekana kubadilisha hadhi, hali na jamii iliyopo katika mji huo mtakatifu wa Jerusalem havitakuwa na athari ya kisheria, na ni batili na ni lazima ubadilishwe," mswada huo umesema.
Wanadiplomasia wanasema wanatarajia Marekani kutumia uwezo wake wa kura ya turufu kuzuwia hatua hiyo wakati , wengi kama sio wote , wajumbe 14 wa baraza la Usalama wanatarajia kuunga mkono mswada huo wa azimio.
Pence kwenda Mashariki ya kati
Makamu wa rais wa Marekani Mike Pence atazuru Jerusalem siku ya Jumatano , akijitumbukiza katika mzozo wa moja kati ya suala lenye utata kabisa katika mzozo kati ya Wapalestina na Israel.
Israel ilichukua udhibiti wa sehemu ya mashariki mwa mji huo katika vita vya mashariki ya kati mwaka 1967 na inaliona eneo lote la mji wa Jerusalem kuwa mji ambao haukugawanyika.
Wapalestina wanaliona eneo la mashariki mwa Jerusalem kuwa mji mkuu wao wa hapo baadaye.
Balozi wa Israel katika Umoja wa mataifa Danny Danon "anashutumu vikali" mswada huo , akipuuzia kwamba ni juhudi za Wapalestina "kuandika upya historia."
"Hakuna kura ama mjadala utakaobadilisha hali halisi kwamba Jerusalem ilikuwa ama itakuwa mji mkuu wa Israel," danon alisema katika taarifa.
Mswada huo wa azimio unatoa wito kwa nchi zote kujizuwia kufungua balozi zao mjini Jerusalem, ukiakisi wasi wasi kwamba serikali nyingine zinaweza kufuata kile Marekani ilichofanya.
Mswada huo unataka kwamba mataifa yote wanachama kutotambua hatua yoyote ambayo itakwenda kinyume na maazimio ya Umoja wa Mataifa kuhusu hadhi ya mji huo.
Maazimio kadhaa ya Umoja wa mataifa yanaitaka Israel kujiondoa kutoka katika ardhi iliyokamata wakati wa vita vya mwaka 1967 na kusisitiza haja ya kufikisha mwisho kulikalia eneo la Wapalestina.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Isaac Gamba