1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSudan

Maelfu waukimbia mji wa Um Rawaba wakati vita vikiongezeka

13 Januari 2025

Maelfu ya watu wameukimbia mji wa Um Rawaba kusini mwa Sudan tangu mapigano yalipozuka wiki iliyopita kati ya jeshi la Sudan na kikosi cha wanamgambo wa RSF.

https://p.dw.com/p/4p5Iw
Sudan Agari | Binnenvertriebene suchen Zuflucht
Watu wakipanga foleni ili kujiandikisha kwa ajili ya kupokea msaada wa chakula katika kambi ya wakimbizi wa ndani (IDP) eneo la Agari, Kordofan Kusini. Picha: Guy Peterson/AFP

Shirika la kimataifa la uhamiaji IOM limesema familia katika kata kati ya 1,000 hadi 3,000 zimeukimbia mji huo katika jimbo la Kordofan Kaskazini  ndani ya siku tano pekee.

IOM imeeleza katika taarifa kuwa, familia hizo zimekimbia kwa kuhofia usalama wa maisha yao kutokana na ongezeko la mapigano katika mji huo. Takwimu za hivi karibuni za Umoja wa Mataifa zinasema kuwa zaidi ya watu 205,000 wamepoteza makaazi yao katika jimbo hilo la Kordofan Kaskazini.

Soma pia:  Hali ya njaa yatishia eneo la Darfur Kaskazini nchini Sudan

Mapigano yalizuka katika eneo hilo wiki iliyopita kati ya jeshi na wanamgambo wa RSF, katika wakati jeshi likiongoza operesheni katika jimbo la Al-Jazira, liliko takriban kilomita 300 upande wa kaskazini mashariki.

Kiongozi wa RSF Mohamed Hamdan Daglo alisema mnamo siku ya Jumamosi kwamba kikosi chake kimepoteza mji mkuu wa jimbo la Al-Jazira, Wad Madani, baada ya jeshi na makundi ya wanamgambo washirika kuingia mjini humo kufuatia zaidi ya mwaka mmoja wa udhibiti wa wanamgambo hao.