UN: Mauaji ya halaiki yaweza kuzuiliwa Sudan Kusini
14 Desemba 2016Mkuu wa Tume ya Umoja wa Mataifa kuhusiana na masuala ya haki za binadamu, amesema jumuiya ya kimataifa bado inayo nafasi ya kuiepusha Sudan Kusini na mauaji makubwa kama ya kimbari yaliyofanyika nchini Rwanda mwaka 1994, ikiwa wanajeshi 4,000 watapelekwa mara moja katika nchi hiyo, na mahakama ikaundwa kuwahukumu watuhumiwa wa mauaji.
''Sudan Kusini inakabiliwa na kitisho cha vita kamili vya wenyewe kwa wenyewe, ambavyo vinaweza kuiyumbisha kanda nzima,'' Yasmin Sooka amekiarifu kikao cha dharura cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva.
Kamishna wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia haki za binadamu Zeid Ra'ad al Hussein ameutaka Umoja wa Afrika kuunda haraka mahakama ambayo ''itaelekeza juhudi katika kuwawajibisha wanaongoza vitendo vya mauaji''.
Machar hayuko kizuizini
Wakati huo huo, Idara ya Uhusiano wa Kimataifa ya Afrika Kusini imekanusha ripoti kuwa kiongozi wa upinzani nchini Afrika Kusini Riek Machar aliondoka nchini humo na kuwasili nchini Ethiopia alikowekwa kizuizini. Msemaji wa idara hiyo, Clayson Monyela, amesema Machar ni mgeni wa nchi hiyo kutokana na maombi ya Jumuiya ya Ushirikiano ya Pembe ya Afrika, IGAD.
Mwezi uliopita, waasi walikuwa wamesema Machar alishikiliwa nchini Ethiopia na kuzuiwa kurejea katika ngome za vikosi vitiifu kwake ambavyo ziko karibu ya mpaka baina ya Ethiopia na Sudan Kusini.
Msemaji wa waasi Dickson Gatluak ameliambia shirika la habari la Ujerumani, DPA kuwa Machar alirudishwa nchini Afrika Kusini Novemba 22 kwa sababu viza yake nchini Ethiopia haikuwa tayari.
Gatluak amethibitisha kuwa Riek Machar hayuko kizuizini, na kuongeza kuwa uhusiano wao na serikali ya Afrika Kusini ni mzuri. ''Serikali ya Sudan Kusini inapenda kumuona Machar akisalia kimya ukimbizini,'' amesema.
Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre, dpae
Mhariri: Grace Patricia Kabogo