1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Mauaji ya Khashoggi yalipangwa na Saudi Arabia

8 Februari 2019

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binaadamu amesema uchunguzi alioufanya umethibitisha mauaji ya mwandishi habari wa Saudi Arabia, Jamal Khashoggi yalipangwa na kutekelezwa na maafisa wa Saudia.

https://p.dw.com/p/3Cyrz
Agnes Callamard Sonderberichterstatterin  UN für außergerichtliche, summarische oder willkürliche Hinrichtungen
Picha: picture-alliance/AP Photo/K. Kadim

Agnes Callamard ameitoa kauli hiyo jana baada ya kumaliza ziara yake maalum nchini Uturuki na anatarajia kuiwasilisha ripoti yake katika Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa mwezi Juni, mjini Geneva, Uswisi. Hata hivyo, uchunguzi wa Callamard na timu yake bado unaendelea.

Callamard amesema Saudi Arabia ilihujumu juhudi za Uturuki kuchunguza mauaji ya Khashoggi, aliyeuawa Oktoba 2 ndani ya ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul. Aidha, ameuita uchunguzi wake kama hatua muhimu kuelekea kwenye ukweli na uwajibikaji.

Amesema ushahidi uliokusanywa unaonesha wazi kuwa Khashoggi aliuawa kikatili na maafisa wa Saudia. Akiwa nchini Uturuki katika uchunguzi huo huru, Callamard alikutana na mwendesha mashtaka mkuu wa nchi hiyo, mkuu wa idara ya usalama pamoja na mawaziri wa mambo ya nje na sheria.

Türkei Istanbul Protest gegen Ermordung von Khashoggi durch Saudis
Picha inayomuonesha Jamal KhashoggiPicha: Getty Images/AFP/Y. Akgul

Hayo yanajiri wakati ambapo Uturuki imesema kukosekana kwa uwazi kutoka kwa maafisa wa Saudia kunaleta wasiwasi mkubwa na kunaondoa uaminifu kwa maafisa hao. Hayo yameelezwa leo na Fahrettin Altun, mkurugenzi wa mawasiliano wa Rais Recep Tayyip Erdogan.

Altun amesema viongozi wa Saudi Arabia wanapaswa kuwakabidhi nchini Uturuki wauaji wa Khashoggi, kama ushahidi wa kuonesha nia yao ya kuzingatia haki, na kuongeza kuwa uchunguzi wa Uturuki katika mauaji hayo, unafanana na ule wa Umoja wa Mataifa.

Wakati huo huo, wabunge wa Marekani wametishia kuchukua hatua kali dhidi ya Saudi Arabia kuhusu mauaji ya Khashoggi, kutokana na taarifa mpya zinazoeleza kuwa mrithi wa kiti cha mfalme wa Saudia, Mohammed bin Salman aliwahi kusema kuwa atatumia ''risasi'' dhidi ya Khashoggi, kama hatorejea nyumbani na kuachana na ukosoaji wake kwa serikali.

Mohammed bin Salman
Mwanamfalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin SalmanPicha: picture-alliance/dpa/SPA

Hayo yameripotiwa jana katika gazeti la New York Times na kwamba Bin Salman aliyatoa matamshi hayo mwaka 2017 wakati akizungumza na msaidizi wake. Gazeti hilo limezinukuu duru kutoka kwa maafisa wa sasa na wa zamani wa Marekani na wale wa mambo ya kigeni ambao wanajua kuhusu taarifa hizo za kijasusi.

Rais wa Marekani, Donald Trump, leo atakabiliwa na kizingiti hicho, ikiwa ni siku ya mwisho aliyopewa na Bunge la Marekani kueleza kama Bin Salman aliamuru mauaji ya Khashoggi. Mwezi Oktoba, Kamati ya Bunge ya Uhusiano wa Kigeni, iliipa serikali ya Trump siku 120 hadi Februari 8, kueleza iwapo mwanamfalme huyo aliamuru mauaji ya Khashoggi na kumtaka achukue hatua dhidi yake.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo, AFP, AP, DPA, Reuters
Mhariri: Daniel Gakuba