1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

UN: Myanmar yaendelea kushuhudia umwagaji damu

4 Machi 2021

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa amesema watu 38 wameuawa wakati vikosi vya usalama vikiripotiwa kuwafyatulia risasi za moto waandamanaji,

https://p.dw.com/p/3qBKB
Myanmar | Demonstration gegen Militärputsch
Picha: REUTERS

Mauaji hayo ya siku moja yakiwa mabaya zaidi tangu kutokea kwa mapinduzi ya kijeshi mwezi uliopita katika nchi hiyo ya Kusini Mashariki mwa Asia.

Christine Schraner Burgener amewaambia waandishi wa habari kuwa watu 38 wameuawa na wengine wengi wamejeruhiwa bila ya kutoa maelezo zaidi.

Soma zaidi: Majirani wa Myanmar washinikiza Suu Kyi aachiwe huru

Mjumbe huyo maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Myanmar ameongeza kuwa zaidi ya watu 50 wameuawa tangu jeshi lilipochukua uongozi.

"Inaonekana wazi kuwa polisi inatumia bunduki na risasi za moto dhidi ya waandamanaji. Kiasi watu 1,200 wamewekwa kizuizini na familia nyingi hazijui pa kuwapata jamaa zao, hawajulikana kama wana afya au la."

Myanmar imeshuhudia ghasia na maandamano tangu Februari 1 baada ya jeshi kumuondoa madarakani kiongozi wa nchi hiyo Aung San Suu Kyi.

Jamii ya kimataifa yalaani mauaji

Myanmar I  Free our Leader Proteste
Picha: STR/AFP/Getty Images

Jamii ya kimataifa imekuwa ikilishinikiza jeshi kurejesha utawala wa kiraia wakati Uingereza ikiitisha mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mnamo siku ya Ijumaa kuzungumzia juu ya kadhia ya nchi hiyo.

Marekani imesema imeshtushwa na ghasia na mauaji yanayotekelewa na vikosi vya usalama vya Myanmar.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani Ned Price amesema:

"Tuna wasiwasi juu ya kuongezeka kwa ghasia, kushambuliwa na kukamatwa kwa waandishi wa habari. Tunatoa wito kwa jeshi kuwaachilia huru mara moja wote waliokamatwa na kuacha kutoa vitisho dhidi ya vyombo vya habari na wengine wanaokamatwa kiholela kwa sababu tu ya kufanya kazi zao"

Wakati hayo yanaarifiwa, mamlaka ya jeshi la Myanmar imewatia hatiani mpiga picha wa shirika la habari la Associated Press pamoja na waandishi wengine wa habari kwa kuripoti juu ya maandamano yanayoendelea nchini humo.

Mpiga picha huyo, Thein Zaw mwenye umri wa miaka 32 alikamatwa katika mji wa kibiashara wa Yangon mnamo siku ya Jumamosi.

Wakili wa Zaw amesema, mpiga picha huyo na waandishi wengine wa habari wameshtakiwa kwa makosa ya kusababisha hofu na kueneza habari za uwongo.

Jeshi lilibadilisha sheria mwezi uliopita na kuongeza adhabu ya makosa ya aina hiyo kutoka adhabu ya miaka miwili hadi miaka mitatu jela.