UN: Taliban bado ina mahusiano na Al-Qaida
2 Juni 2020Makubaliano ya amani kati ya Taliban na Marekani yaliyosainiwa nchini Qatar mnamo mwezi Februari yalikusudiwa kuwaruhusu wanajeshi wa Marekani kuondoka Afghanistan kwa awamu baada ya miaka 19 ya vita jambo ambalo lingefungua njia kwa mazungumzo ya ndani na kutoa mwelekeo wa mustakabali wa kisiasa wa nchi hiyo.
Chini ya makubaliano hayo, Taliban iliahidi kupambana na makundi mengine ya kigaidi likiwemo al-Qaida, ambalo awali waliwahi kulilinda na kuwazuia wanajeshi kutumia eneo la Afghanistan kupanga mashambulizi dhidi ya Marekani.
Usiri katika kulinda operesheni za kiintelijensia
Hata hivyo maelezo zaidi kuhusu wajibu wa Taliban katika kukabiliana na ugaidi hayakuwahi kuwekwa hadharani. Mjumbe wa amani wa Marekani na mmoja wa waasisi wa makubaliano hayo Zalmay Khalilzad, anasema kuwa ni muhimu kuwa na hali ya usiri ili kulinda operesheni za kiintelijensia zinazohusika katika kuyatekeleza makubaliano hayo.
Khalilzad aliwaambia wandishi wa habari mjini Washington kuwa ahadi ya Taliban ilikuwa maalumu "kuanzia katika uwepo wao, namna ya mafunzo, na namna ya kuajiri, kuchangisha fedha na hata namna ya udhibiti.''
Alisisitiza kuwa wamefanikiwa pakubwa katika mkataba huo na hatua za baadaye katika kupunguza vikosi nchini Afghanistan zitategemea namna Taliban itakavyotekeleza ahadi zao.
Kamati ya Umoja wa Mataifa iliyotoa ripoti hii imesema wanachama kadhaa muhimu wa al-Qaida waliuawa katika miezi kadhaa iliyopita lakini baadhi ya viongozi wa ngazi ya juu wa kundi hilo, lililowahi kuongozwa na Osama bin Laden, bado wapo Afghanistan.
Kundi la Taliban lahusishwa pia na mtandao wa Haqqani
Ripoti hiyo imesema kundi hilo lina mafungamano na mtandao wa Haqqani ambalo ni washirika wa Taliban na bado lina wajibu muhimu katika operesheni za Taiban.
Jihadi, ama vita vitakatifu, ni historia inayoendelea kuyaunganisha makundi hayo mawili ya wabeba silaha. Viongozi kadhaa wa juu wa al-Qaida, kama vile Ayman al-Zawahri ambaye alimrithi bin Laden kama kiongozi wa mtandao huo wanahusishwa na vita vya miaka ya 1980 vya Afghanistan dhidi ya uvamizi wa muungano wa zamani wa kisovieti, wakati wapiganaji wa vita vitakatifu wa Afhghanistan walipokuwa wakifadhiliwa na Marekani ili kuwaondoa wanajeshi wa Urusi.
Taliban haikupatikana kutoa maoni juu ya ripoti ya Umoja wa Mataifa. Lakini wakosoaji wameonesha wasiwasi kuhusu mkataba kati ya Marekani na kundi hilo na kuonya kuwa makubaliano hayo yanaweka ugumu katika kuyafuatilia makundi ya waasi.
chanzo: AP