UN yaiwekea vikwazo Korea kaskazini
23 Desemba 2017Baraza hilo kwa kauli moja liliidhinisha azimio lililotayarishwa na Marekani ambalo pia linaamuru kurejeshwa kwa wafanyakazi wa Korea Kaskazini waliopelekwa nje ya nchi hiyo kupata mapato ambayo ni kwa ajili ya utawala wa Kim Jong-Un.
Ni vikwazo vya tatu kuwekwa dhidi ya Korea kaskazini mwaka huu na vinakuja wakati Marekani na Korea kaskazini hazioneshi ishara ya kuwa tayari kuanzisha mazungumzo juu ya kumaliza mzozo huo katika rasi ya Korea. Rais wa Marekani Donald Trump Ijumaa liisifu hatua hiyo, akisema jumuiya ya kimataifa inataka kuleta amani na utawala huo uliotengwa.
"Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipiga kura 15-0 kuunga mkono vikwazo vya ziada dhidi ya Korea kaskazini. Dunia inataka amani , sio kifo!" aliandika Trump katika ukurasa wa Twitter.
Azimio hilo linapiga marufuku upelekaji wa karibu asilimia 75 ya bidhaa za mafuta yaliyosafishwa nchini Korea Kaskazini , kuweka ukomo katika upelekaji wa mafuta ghafi na kuwaamuru raia wote wa Korea kaskazini wanaofanyakazi nje ya nchi kurejeshwa nyumbani ifikapo mwishoni mwa mwaka 2019.
Mswada wa Marekani
Marekani iliwasilisha mswada wa azimio hilo siku ya Alhamis kufuatia majadiliano na China, mshirika mkubwa wa Korea kaskazini na nchi ambayo ndio inayosafirisha mafuta kwa wingi nchini humo.
Akieelezea Korea Kaskazini kama "mfano mkubwa wa kusikitisha wa uovu katika dunia ya sasa," balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley amesema vikwazo hivyo vipya "vinaakisi hasira ya jumuiya ya kimataifa dhidi ya hatua za utawala wa Kim. Azimio hilo " linatuma ujumbe wa wazi kwa Pyongyang kwamba ukaidi zaidi utakaribisha adhabu zaidi na kutengwa," amesema balozi huyo.
Hatua hizo zinakuja kutokana na majaribio ya Korea ya Kaskazini ya makombora ya masafa marefu ICBM hapo Novemba 28 ambapo ilionekana kuwa ni hatua kubwa iliyopigwa na Korea Kaskazini katika jaribio lake la kuitishia Marekani kwa mashambulizi ya kinyuklia.
Trump alitishia "kuivuruga kabisa " Korea Kaskazini iwapo itaishambulia Marekani wakati Korea Kaskazini inasisitiza kwamba dunia lazima ikubali kwamba nchi hiyo ni moja kati ya nchi zenye silaha za kinyuklia.
Korea kaskazini yapunguziwa kuuziwa mafuta
Mwezi uliopita , Trump alimtaka rais wa China Xi Jinping kuacha kuipelekea mafuta Korea Kaskazini, hatua ambayo ingedhoofisha uchumi wa nchi hiyo ambao unamatatizo. Upelekaji mafuta ghafi umepunguzwa hadi mapipa milioni nne kwa mwaka na ukomo wa mapipa 500,000 ya bidhaa za mafuta yaliyosafishwa, ikiwa ni pamoja na dizeli na mafuta ya taa, yanayotarajiwa kupelekwa mwakani, ni chini kutoka mapipa milioni mbili katika vikwazo vilivyopita.
Iwapo Korea Kaskazini itafanya jaribio jingine la kinyuklia ama majaribio ya makombora ya masafa marefu ICBM, "baraza la Usalama litachukua hatua nyingine kuzuwia mauzo mengine kwa nchi hiyo ya petroli," limeeleza azimio hilo.
Marekani ililenga hapo awali kutaka kuwafukuza katika muda wa mwaka mmoja mamia kwa maelfu ya wafanyakazi wa Korea Kaskazini, wengi wao wakifanyakazi nchini Urusi na China, lakini muda huo wa mwisho ulirefushwa hadi miaka miwili baada ya Urusi kupinga.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Yusra Buwayhid