1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yataka usitishaji mapigano kupisha chanjo kwa watoto Gaza

Angela Mdungu
16 Agosti 2024

Umoja wa Mataifa umeomba mapigano yasitishwe kwa muda katika kipindi cha siku saba kwenye Ukanda wa Gaza ili kutoa nafasi kwa zaidi ya watoto 640,000 kupewa chanjo dhidi ya ugonjwa wa polio.

https://p.dw.com/p/4jZ0t
Gazastreifen El-Zawaida | Polio-Impfungen in Gaza
Picha: Omar Ashtawy/APA Images/Zumapress/picture alliance

Ugonjwa huo umegunduliwa kuwepo katika maji taka ya Ukanda huo. Shirika la afya la Afya duniani WHO limesema kuwa, mashirika ya Umoja wa Mataifa yanataka kutoa chanjo hiyo ya matone kwa watoto wenye umri chini ya miaka kumi kuanzia baadaye mwezi huu.

Limeongeza kuwa bila kuwepo kwa usitishwaji wa muda wa mapigano kwa ajili ya kutoa huduma za kiutu, ufikishwaji wa chanjo hizo hauwezi kufanikiwa.

UN yalaani shambulio la walowezi Ukingo wa Magharibi

Katika hatua nyingine, Umoja wa Mataifa umesema kuwa shambulio baya la walowezi katika kijiji kimoja kwenye Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu na Israel lilikuwa la kutisha na kwamba kuna hali ya mamlaka kutokujali mashambulizi ya aina hiyo.

Akilizungumzia pia tukio hilo mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amesema atapendekeza kuwawekea vikwazo wawezeshaji wa vurugu hizo

Kupitia ukurasa wake wa Jukwaa la X, Borrell amesema kuwa siku hadi siku walowezi wa Israel wamekuwa wakichochea vurugu katika eneo hilo na kuchangia kuhatarisha uwezekano wa kupatikana kwa amani.

Amesema serikali ya Israel inapaswa kuzuia vitendo hivyo mara moja. Vikwazo  vinavyopendekezwa na Borrell vitahitaji kuidhinishwa kwa sauti moja na mataifa yote 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya yenye mgawanyiko kuhusu mzozo wa Israel na Palestina.

Soma zaidi: Shambulizi la Israel laua watano Ukingo wa Magharibi

Hayo yanajiri wakati awamu mpya ya  juhudi za kimataifa za usuluhishi zikiendelea huko Qatar kwa siku ya pili. Mazungumzo yanafanyika huku mawaziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza David Lammy na Stéphane Séjourné wa Ufaransa wakiwa  ziarani Jerusalem kuhamasisha upatikanaji wa makubaliano ya kusitisha vita Gaza.

Stéphane Séjourné
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa Stéphane Séjourné aliye ziarani JerusalemPicha: JOSEPH EID/AFP

Kwa upande wake Waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza ametoa wito wa kusitishwa kwa mapigano mara moja, kuachiliwa kwa mateka, kuwalinda raia na kuhakikisha upatikanaji wa njia salama kwa ajili ya misaada ya kiutu

Mbali na ziara hiyo, watu wawili wameuwawa Ijumaa baada ya Israel kufanya shambulio la anga lililolilenga jengo moja katika eneo la Al-Nuseirat katikati mwa Gaza. Idadi ya majeruhi haijajulikana.