UN yapunguza mgao wa chakula Yemen kutokana na ukata
22 Desemba 2021Taarifa iliyotolewa na shirika hilo la mpango wa chakula imeeleza kuwa familia ambazo zipo kwenye orodha ya kupata msaada wa chakula zitapata takriban nusu ya mgawo ambayo ndio kiwango cha chini kinachotolewa na WFP.
Misaada mingine ambayo itakuwa mashakani kukumbwa na changamoto hiyo ni pamoja na miradi ya kupambana na utapiamlo kwa watoto.
Mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo hilo la mpango wa chakula WFP yalionya mapema mwaka huu juu ya uwezekano wa kupunguza shughuli zake kutokana na kupokea kiasi cha fedha kisichokidhi mahitaji.
Soma pia: Waasi 40 wa Houthi wauwawa kwenye mapigano Yemen
Wafadhili wamechangia kiasi cha dola bilioni 2.68 hadi kufikia mwezi Oktoba, badala ya kiasi cha dola bilioni 3.85 zilizohizajika kufikia malengo ya programu za mashirka hayo.
Katika taarifa yake mkurugenzi wa kanda wa WFP Corinne Fleischer, amesema akiba ya WFP nchini Yemen inapungua kwa kasi sana na kila mara wanavyopunguza chakula wanafahamu kuwa watu wengi ambao tayari wana shida na uhaba wa chakula wataungana na kundi la mamilioni ambao wanakufa njaa.
Watu wapatao milioni tano ambao wapo katika hatari kubwa zaidi ndio watasalia na mgao kamili kutoka katika shirika hilo la Umoja wa Mataifa ambalo limekuwa likitoa msaada wa chakula nchini Yemen.
WFP imeongeza kuwa hadi sasa inalisha takriban watu milioni 13 kwa mwezi katika taifa hilo la Mashariki ya Kati.
Kitisho cha baa la njaa
Yemen iliyogawanyika kati ya kundi la Houthi lenye mfungamano na Iran iliopo kaskazini mwa nchi hiyo na serikali inayotambulika kimataifa iliyo upande wa kusini mwa nchi, imetumbukia katika baa la njaa kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka saba sasa.
Soma pia: Saudi Arabia na vita visivyo mwisho Yemen
Sababu ya hali hiyo ni pamoja na mfumuko mkubwa wa bei unaosababishwa na kushuka kwa thamani ya fedha pamoja na vikwazo vya uagizaji bidhaa kutoka nje.
Vita hivyo vimeua maelfu ya watu wengi wao wakiwa ni raia na kuwaacha mamilioni katika baa la njaa.
Mnamo mwezi Juni, WFP ilianza tena kutoa misaada ya chakula ya kila mwezi katika baadhi ya maeneo yanayodhibitiwa na Wahouthi ikiwa ni baada ya kupunguza ugawaji wa kila mwezi kutoka Aprili 2020 kutokana na wafadhili kuacha kutoa fedha.
Tayari Benki ya Dunia imeidhinisha kiasi cha dola milioni 170 kama msaada kwa Yemen kwa ajili ya miradi ya misaada ya chakula vijijini, miundombinu na mazingira.
Chanzo: Mashirika