UN yapuuza vitisho vya Trump kuhusu Jerusalem
22 Desemba 2017Kura hiyo isiyofungamanisha kisheria iliyoitangaza hatua ya Marekani kuhusu Jerusalem kuwa batili, iliungwa mkono na mataifa 128 dhidi ya 9, huu ukiwa ni ushindi kwa Wapalestina, lakini usiyo mkubwa kama ilivyokuwa imebashiriwa.
Kufuatia vitisho vya Marekani, mataifa 35 kati ya 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa yalijizuwia kupiga kura na wawakilishi wa mataifa 21 hawakuwepo.
Azimio hilo lilithibitisha msimamo wa muda mrefu wa Umoja wa Mataifa juu ya mji huo mtakatifu tangu mwaka 1967: Kwamba hadhi ya mwisho ya Jerusalem laazima iamuliwe katika mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Israel na Wapalestina.
Utawala wa Trump ulibainisha wazi kwamba kura hiyo haitoathiri mpango wake wa kuhamisha Ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv kwenda Jerusalem. Na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema baadae kwamba anaikataa kabisaa kura hiyo alioitaja kuwa upuuzi.
Balozi wa Palestina Riyad Mansour aliitaja kura hiyo kuwa ushindi si tu kwa wapalestina, lakini pia kwa Umoja wa Mataifa, na sheria ya kimataifa, na kuongeza kuwa Balozi wa Marekani Nikki Haley alishindwa vibaya, kwa kuweza kuyashawishi mataifa saba tu mbali na Marekani na Israel kupinga azimio hilo.
Marekani na Israel ziliendesha kampeni kubwa ya ushawishi dhidi ya azimio hilo, huku Balozi Halley akituma barua kwa zaidi ya mataifa 180 akionya kwamba wataandika majina ya watakaopiga kura dhidi ya Marakani. Trump alikwenda hata mbali zaidi kwa kutishia kukata misaada: "Waache wapige kura dhidi yetu. Tutaokoa fedha nyingi. Hatujali," alisema.
Wapokeaji wakubwa misaada wamgeuka mfadhili wao
Lakini mwishowe, mataifa yanayopokea msaada zaidi kutoka Marekani, yakiwemo Afghanistan, Misri, Jordan, Pakistan, Nigeria, Ethiopia, Tanzania na Afrika Kusini yaliunga mkono azimio la Umoja wa Mataifa.
Mataifa tisa yaliopiga kura ya hapana yalikuwa Marekani yenyewe, Israel, Guatemala, Honduras, Micronesia, Nauru, Palau na Visiwa vya Mashall na Togo.
Miongoni wa nchi zilizojizuwia ni Australia, Argentina, Canada, Colombia, Croatia, Jamhuri ya Czech na Mexico, huku Kenya, ambayo ndiyo ya tano kwa kupokea msaada mkubwa wa Marekani mwaka ulipiota, Georgia na Ukraine ambazo zote zina uhusiano wa karibu na Marekani zikikosekana.
Mhariri wa musuala ya usalama wa taifa wa shirika la habari la Marekani - Associated Press Brad Klapper, anasema inasubiriwa kuona athari za kura hiyo juu ya uhusiano wa Trump na Umoja wa Mataifa.
"Haijabainika wazi nini ilikuwa athari ya vitisho hivyo, lakini kwa vile vimetolewa, haijulikani namna utawala wa Trump unavyopanga kuvitekeleza, ikiwa utavitekeleza," alisema Clapper.
Baada ya kura hiyo, Balozi Haley aliweka picha kwenye ukurasa wa twitter, akizitaja nchi 65 zilizopiga kura ya hapana, kujizuwia na zisizokuwepo na kusema: Tunazishukuru nchi hizi kwa kutojihusisha na kile alichokiita njia zisizo za uwajibikaji za Umoja wa Mataifa.
Baadae alituma mwaliko kwa mabalozi 65 wa mataifa hayo akiwaalika kwenye hafla Janurari 3 kuwashukuru kwa urafiki wao na Marekani.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape,rtre.
Mhariri: Saumu Yusuf