1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yatafuta dola milioni 910 kusaidia Nigeria kaskazini

22 Januari 2025

Umoja wa Mataifa unatafuta dola milioni 910 kwa ajili ya kutoa msaada wa kibinadamu unaohitajika haraka kusaidia watu kaskazini mwa Nigeria.

https://p.dw.com/p/4pTwH
Nigeria Maiduguri | Mafuriko nchini Nigeria
Nigeria Maiduguri | Mafuriko nchini NigeriaPicha: Ahmed Kingimi/REUTERS

Umoja wa Mataifa umesema wiki hii utatoa rai ya kuchangishwa dola 910 za kimarekani ili kusaidia kukabiliana na migogoro ya kibinadamu katika eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria ambalo limekuwa katika mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa waasi tangu mwaka 2009 huku eneo hilo pia likitajwa kuathirika na mafuriko mabaya ya mwaka uliopita.

Nyaraka za Umoja wa Mataifa zilizooneshwa kwa shirika la habari la Reuters zimesema takriban watu milioni 7.8 wanahitaji msaada wa kiutu katika majimbo matatu ya kaskazini mashariki mwa Nigeria ya Adamawa,Borno na Yobe, na Umoja wa Mataifa unalenga kuwasaidia watu milioni 3.6 kati yao.

Soma pia: Shirika la MSF laonya kuhusu mgogoro wa kibinadamu Nigeria

Ripoti ya pamoja ya serikali ya Nigeria na Umoja wa mataifa ya mwezi Novemba mwaka uliopita ilisema Nigeria inakabiliwa na mzozo mbaya zaidi wa njaa duniani na kwamba zaidi ya watu milioni 30 wanatarajiwa kukabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula mwaka huu.

Hapo awali Umoja wa Mataifa ulisema kuwa hali mbaya iliyopo kaskazini mashariki mwa Nigeria inazidi kusahaulika kwa sababu macho na masikio ya wengi yalihamia kwenye mizozo mingine duniani kama vile vita huko Ukraine, Gaza na Sudan.