UN yatahadharisha kuhusu hali ya mabwawa mengine 2 Libya
18 Septemba 2023Hayo yanajiri mnamo wakati juhudi za uokozi zikiendelea, ambapo hadi sasa maelfu ya watu wamethibitishwa kufariki na zaidi ya 10,000 bado hawajulikani waliko tangu kutokea Kimbunga Daniel kilichosababisha maafa makubwa mnamo Septemba 10 nchini humo.
Kulingana na shirika la misaada la Umoja wa Mataifa, OCHA, mabwawa yanayowatia tumbo joto ni lile la Jaza, lililoko kati ya mji ulioharibiwa pakubwa wa Derna na mji wa Benghazi. Jingine ni bwawa la Qattara lililoko karibu na mji wa Benghazi.
Libya imekumbwa na mafuriko ya kiwango cha tsunami yaliyosababisha majanga makubwa pamoja na vifo
Hata hivyo, shirika la OCHA limesema kumekuwa na taarifa zinazotofautiana kuhusu mabwawa hayo. Shirika hilo limewanukuu wasimamizi wa mabwawa hayo waliosema kuwa, yote yako katika hali nzuri na yanafanya kazi vyema, na kwamba yalikuwa yanawekewa mabomba ili kupunguza maji.
Wito watolewa wa misaada zaidi
Huku juhudi za kuwatafuta manusura na pia miili zaidi, mkuu wa shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR nchini Libya, Rana Ksaifi, ametoa ombi la misaada zaidi, akielezea kuwa hali ni ya kutisha.
"Timu za uokozi zinaendelea kujaribu kuokoa maisha. Lakini hali bado ni tete kwa sasa. UNHCR tayari imetoa vifaa vya msingi kwama hatua ya kwanza na la kwanza na tunafany akazi na washirika wetu wa ndani kupunguza athari kwa familia zinazoendelea kukum,bwa na mshtuko mkubwa. Lakini mahitaji na msaada zaidi vinahitajika kwa dharura," amesema Ksaifi.
Kwingineko Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (IRC), limetahadharisha leo kwamba maeneo yaliyopigwa na mafuriko mashariki mwa Libya yapo katika hatari ya kukabiliwa na mgogoro wa kiafya, hususan mji wa bandari wa Derna.
Manusura wa mafuriko Libya wakabiliwa na uhaba wa maji safi
Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, IRC imesema mafuriko ya hivi karibuni yamechanganya maji taka na yale ya matumizi ya kila siku, hali inayowaweka watumiaji wa maji hayo katika hatari kubwa kiafya.
IRC imesema tayari imerekodi watoto wasiopungua 55 ambao wameugua mjini Derna kwa sababu ya kutumia maji yaliyochafuka.
Mji wa Derna uliharibiwa pakubwa wiki iliyopita kufuatia Kimbunga Daniel kilichosababisha mvua kubwa. Mabwawa mawili yaliporomoka na kusababisha vifo vya maelfu ya watu. Hadi sasa maelfu ya watu pia bado hawajulikani waliko. Maafisa hawajatoa takwimu kamili.
Mkanganyiko kuhusu idadi ya vifo
Hapo awali shirika la OCHA lilikadiria kuwa watu 11,300 wamefariki dunia na kwamba wengine 10,100 walikuwa hawajulikani waliko. OCHA lilisema takwimu hizo ni kulingana na shirika la Hilal Nyekundu, lakini msemaji wa Hilal Nyekundu alipinga takwimu hizo.
Baadaye OCHA lilifutilia takwimu ya awali badala yake lilitaja takwimu ya Shirika la Afya Duniani WHO lililosema idadi ya watu waliokufa hadi sasa ni 3,958 na wale ambao bado hawajulikani waliko ni zaidi ya 9,000.
Usiku wa kuamkia Jumatatu, waziri wa afya katika serikali pinzani ya Libya Abdel Jalil aliwaambia waandishi habari kwamba idadi ya waliozikwa hadi sasa ni 3, 283.
Mapema wiki iliyopita, Meya wa mji wa Derna alisema kulikuwa na uwezekano kwamba hadi watu 20,000 wameuawa kwenye janga hilo.
Vyanzo: DPA, EBU